AINA ZA UWEKEZAJI KATIKA HISA

Muwekezaji

Mgeni
Dec 10, 2021
10
3
5
Dar Es Salaam
Kuna wafugaji wanapenda sana kununua ndama kule mnadani (minada mingi ya vijijini huwa zinauzwa ng'ombe, mbuzi na kondoo) kwaajili ya kuwakuza na kuja kuwaletea faida hapo baadae lakini kuna wale wafugaji ambao hupenda kununua ng'ombe ambao tayari ni wakubwa lakini mara nyingi huwa ni kwaajili ya maziwa ambao pengine hawakui tena!

Hivyohivyo kwa upande wa wafugaji wa kuku, kuna wanaonunua kuku vifaranga ili wawakuze waje kuzaliana zaidi na kuna wanaonunua kuku kwaajili ya mayai na kuna wanaonunua kuku kwaajili ya kupata nyama tu!

Hivyo basi kama unanunua kuku wa mayai usitegemee atakuwa na nyama nzuri sana kuliko yule kuku wa nyama. Hivi ndivyo pia wawekezaji katika hisa wanavyofanya.

Kuna wawekezaji hupenda kununua hisa zinazokua (Growth Stocks) na kuna wanaopenda kununua hisa kwaajili ya gawio (Dividend Stocks), hisa kama za TBL, TCC ni hisa ambazo hazikui tena lakini ni hisa nzuri kwa gawio (hizi ndiyo hisa zinazotoa gawio kubwa Tanzania) lakini hisa za kampuni kama CRDB, TPCC, NICOL ama NMB ni hisa ambazo zinakua (bei na thamani zitaongezeka) hivyo ni nzuri kwa mwekezaji mwenye malengo ya muda mrefu.

Hivyo mwekezaji anapoenda sokoni analazimika kuchagua, kuwekeza kwenye hisa zinazokua ama kwenye hisa ambazo zitampatia gawio kila baada ya miezi 6 ama miezi 12. Mwekezaji anashauriwa kuwa na malengo kabla ya kuwekeza, malengo hayo yaweza kuwa ya muda mfupi (kupata gawio) na malengo ya muda mrefu (kusubiri hisa zipande bei zaidi ya alivyonunua) na aweze kuziuza na kupata faida.