Chilunda bado ana jambo na Wahispania

Amir

Mgeni
Dec 10, 2021
736
12
5
tanzania
1642057906639.png
Unguja. MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Shaaban Chilunda bado ana machungu na klabu ya Tenerife ya Hispania akisema mabosi wa timu yake hiyo ya zamani ndio waliomharibia dili la timu mbili zilizokuwa zikimuhitaji.

Akizungumza na gazeti hili Chilunda alisema kuwa baada ya mambo kwenda hovyo nchini Hispania alipata ofa za timu mbili nchini Misri na moja ya timu iliyomuhitaji ni ile anayoichezea Himid Mao ya Ghazl El Mahalla SC yenye maskani yake huko El Mahalla El Kubra.

Alisema kuwa hali iliyokuwepo kati yake na waajiri wake hao wa zamani ndiyo iliyosababisha avunje mkataba wake ambapo alipeleka malalamiko yake kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ili asaidiwe kupata barua ya kuachwa.

Alisema kuwa alikuwa tayari kuacha pesa anayodai na kikubwa alichokuwa anakipigania ni hiyo barua pekee ili akacheze katika moja ya timu mbili alizokuwa amepewa ofa.

“Nilichowaambia wao wanipe barua tu, maana hata stahiki zangu nilikuwa sipati tofauti na mkataba ulivyokuwa ukieleza, niliona ni vyema nikatafute maisha sehemu nyingine lakini siwezi kuondoka pasipo kupewa batua ya kuniacha huru.

“Hilo ndilo jambo lililonifanya sasa niende Fifa ili waone namna gani ya kunisaidia maana mwanzo nilitaka barua tu ya kuthibitisha kuwa nipo huru lakini baadaye walijua kuwa nimepata timu sehemu nyingine ambako sasa walikwenda kuharibu mipango na hao wakawa na hofu tena ya kunisajili.

“Nilipoona wameniharibia basi nilirudi Fifa kufungua kesi ya madai ya stahiki zangu ambazo ni pesa ninazowadai, sijalipwa hadi sasa ila naamini nitalipwa maana ni haki yangu. Kiukweli hali hiyo iliniondoa mchezoni hivyo niliamua kurudi nyumbani kupumzisha akili,” alisema.

Alisema baada ya kufika nyumbani timu pekee aliyoona inamfaa ni Azam FC kwa kile alichoeleza kuwa; “Nimelelewa na hii timu, ni timu ya maisha yangu na ninaifahamu vizuri hivyo sijaona wapi niende zaidi ya hapa wakati nasubiri mipango mingine.

“Naamini nitafanikiwa tena kucheza soka la kulipwa, sijakata tamaa juu ya hilo maana moja ya timu ambazo zilinipa ofa hiyo ni hii anayoichezea Himid na nilikuwa tayari kabisa kucheza soka huko,” alisema

Kuhusu mwenendo wa timu yao, Chilunda alisema kwa kusaidiana na wachezaji wenzake anaamini wataivusha Azam FC hapo ilipo na kuwa timu bora zaidi ingawa matokeo yao ya sasa hayawafurahishi.