Lijue Soko la Hisa la Dar-es-Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)

tototundu

Kaka Mkubwa
Nov 26, 2021
23
21
6
Soko la Hisa ni soko ambalo huwezesha hisa, hatifungani na dhamana zingine zilizoorodheshwa katika soko hilo kuuzwa na kununuliwa. Bidhaa hizi huitwa dhamana au kwa lugha ya kigeni (securities). Soko la hisa hapa Tanzania limeanzishwa mwaka 1996 kama kampuni binafsi yenye dhima (limited by guarantee); kwa maana ya kwamba wanachama wa soko hawatakiwi kuweka mtaji wowote. Mwanzoni kulikuwa na wanachama 11 ambao ni madalali wa soko la hisa pamoja na wawekezaji wakubwa (Institutional investors). Soko la hisa lilianza kazi zake rasmi mwezi April mwaka 1998 wakati hisa za TOL Ltd zilipoorodheshwa na kuanza kuuzwa na kununuliwa. Soko la hisa ni soko ambalo linajiendesha lenyewe likisimamiwa na Baraza la Wadhamini (DSE Council).

Tembelea tovuti yao > https://www.dse.co.tz/

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ni nini?

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha na Uchumi iliyoanzishwa na Sheria namba 5 ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya mwaka 1994 ili kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa Tanzania. Majukumu makubwa ya Mamlaka yameainishwa kwenye kifungu namba 10 cha Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana.

Majukumu hayo ni pamoja na:

a) Kuanzisha na kuendeleza masoko ya mitaji Tanzania;
b) kuidhinisha uanzishwaji wa masoko ya hisa na mifuko ya uwekezaji wa pamoja, na kutoa leseni kwa wataalamu wa masoko ikiwa ni pamoja na madalali, wachuuzi, wawakilishi wao, washauri wa uwekezaji, n.k.
c) Kusimamia masoko ya mitaji pamoja na wataalamu wote wanaohusika na utendaji wa masoko hayo; na 2
d) Kuishauri Serikali kwenye masuala yote yahusuyo masoko ya mitaji na dhamana.

Kuna tofauti gani kati ya Soko la Hisa la Dar-es-Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)?

Mamlaka (CMSA) ni taasisi ya serikali, ambayo ilianzishwa na Sheria ya Bunge ili kusimamia masoko ya mitaji na dhamana. Mamlaka imepewa jukumu la kuanzisha na kusimamia masoko haya nchini. Katika kutekeleza wajibu wake, Mamlaka ilianzisha Soko la Hisa la Dar es salaam mwaka 1996 na kusimamia uendeshaji wa soko hilo kwa mujibu wa sheria.

Pia Mamlaka ndiyo inayotoa leseni kwa washiriki wa soko la hisa kama vile madalali, washauri wa uwekezaji na kuidhinisha uanzishwaji wa masoko ya hisa. Mamlaka pia ina mamlaka kwa mujibu wa Sheria kusimamia utendaji wa soko la hisa kwa kutoa maelekezo pale inapobidi kwa Baraza la Wadhamini la DSE.

Wajumbe wa Bodi ya CMSA huteuliwa chini ya kifungu cha 6 kifungu kidogo cha 3 cha sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania humteua mwenyekiti na wajumbe wengine 5 huteuliwa kutokana na nyadhifa zao kama Gavana wa Benki Kuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msajili wa Makampuni na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka. Wajumbe wengine 4 waliobaki huteuliwa na Waziri wa Fedha kwa kuzingatia utaalamu wao kwenye fani ya sheria, uhasibu, fedha na uchumi. DSE inaongozwa na Baraza la Wadhamini (Wakurugenzi) ambao wako 10. Wadhamini hawa wanawakilisha taasisi za fedha kama mifuko ya pensheni, madalali wa soko la hisa, kampuni zilizoorodheshwa katika soko, mwakilishi wa umma wa wawekezaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE.