SPOTI DOKTA: Kumwadhibu zaidi Zouma ni mbaya kiafya

mhariri

Mpiga Chabo
Dec 17, 2021
203
0
0
Zouma oic

WIKI iliyopita habari kubwa katika Ligi Kuu England (EPL), ilimhusu beki wa kati wa klabu ya West Ham, Kurt Zouma ambaye video iliyosambaa mitandaoni ilimwonyesha akimpiga teke paka wake na kumrusha.
Mara baada ya tukio hilo ambalo video hiyo ilitolewa na gazeti maarufu la The Sun kuiweka katika mtandao wake, beki huyo aliomba msamaha na kujutia kitendo alichofanya. Klabu yake tayari imemchukulia hatua kwa kumkata mshahara wa wiki mbili unaofikia Pauni 250,000 na kukipeleka kwa watetezi wa haki za wanyama wajulikanao kama PSRCA.
Pamoja na tukio hilo lililoonyesha ukatili kwa wanyama, Zouma alikuwamo katika kikosi cha kwanza kilichocheza dhidi ya Watford na kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Wakereketwa wa tukio hilo walizidi kujawa na hasira wakikosoa kitendo cha kocha wa West Ham United, David Moyes kumpanga katika kikosi hicho jambo hili likiwa bado bichi.
Moyes alijibu akisema amefanya hivyo akilenga kushinda na si vinginevyo, akieleza Zouma mwenye umri wa miaka 27 hajakamilika kama binadamu wengine. Alieleza kuwa alilofanya ni kosa, akakiri, akajutia hivyo anapaswa kusamehewa kama binadamu. Zouma aliomba msamaha hadharani na kujutia tabia yake hiyo isiyofaa.
Pamoja na yote hayo Zouma pia amekumbana na nyundo nyingine ya wadhamini kampuni ya Adidas ambao wametangaza kujitoa katika dili na beki huyo wakidai sababu ni kitendo hicho. Wakati hayo yakiendelea wadhamini wengine nao wa klabu hiyo nao wanalichunguza tukio hilo ili kujitafakari na udhamini wa klabu na uhusiano wao.
Kama vile haitoshi tayari kuna kusanyo la sahihi 150,00 yaani ‘petition’ linalotaka mchezaji huyo ashtakiwe. Klabu na taasisi ya PSRCA imechukua hatua tayari. Msemaji wa taasisi ya watetezi ya wanyama - RSPCA amesema tayari imewachukua paka wawili waliokuwa wanafungwa na Zouma na wapo katika ungalizi maalumu. Zouma aliendelea kukumbana na mashambulizi mengi hasa mashabiki walioumuona akicheza katika mchezo huo kwani hawakutegemea kama angepangwa katika mchezo dhidi ya Watford.
Kwa upande wa jicho la kitabibu linaona hiyo inatosha na sio sahihi kuendelea kumwadhibu zaidi hatua za awali zilizochukiliwa dhidi yake zinatosha kumfunza. Akiandamwa zaidi hilo linaweza kumpata. Ukijaribu kuvaa viatu vya Zouma kwa sasa na yanayoendelea mitandaoni inaweza kumuathiri kisaikolojia na pengine akaumia kihisia hatimaye afya yake ya akili ikayumba.
Kuendelea kushambuliwa kwa tukio hilo anaweza hata kupata tatizo la sonona, yaani kitabibu depression. Hali kama hiyo inaweza kumfanya mtu akawaza hata kujiua. Mchezaji akishapata matatizo ya kiakili ni vigumu kutimiza majukumu yake uwanjani na kuleta mafanikio.
Kitendo alichofanya kocha Moyes kwa upande wa kitabibu ni faida kubwa kwa Zouma kwani kinampa faraja kuwa pamoja na makosa aliyofanya kipaji chake ni muhimu katika mafaniko ya timu. Moyes ni kama amemtibu kisaikolojia Zouma kwani mtenda kosa huwa katika huzuni huku akijutia kosa. Ni dhahiri kocha huyo aliongea naye vya kutosha kabla ya kuamua kumpanga katika mechi.
Hawa ndio wanaitwa mameneja, uamuzi wao huwa ni mgumu. Wanaamua kwa maslahi ya timu huku wakitambua kuwa bila wachezaji hakuna ushindi. Kwa nchi za Magharibi ni utamaduni wao kutambua haki za wanyama na kuzuia ukatili kwa wanyama, ndege na wadudu. Hata nchi za dunia ya tatu za Afrika nazo zinazibeba sheria hizo katika nchi zao.
Ni kweli kitendo alichoanya Zouma ni kosa, lakini sio sawa kuendelea kumuandama kwani kunaweza kumletea shida ya kiakili jambo ambalo litakuwa hasara kwake na klabu yake. Mwandishi mkongwe Fred Ndesanjo Macha aliwahi kuandika katika moja ya makala zake akieleza namna watu wenye tamaduni za Magharibi wanavyothamini haki za wanyama.
Alitoa mfano yeye akiwa kijana alipokosana na rafiki yake wa kike Mzungu pale alipochukua fimbo na kumpiga nyoka aliyekuwa mazingira jirani nao. Zouma anayetoka Ufaransa ni mkosaji kama binadamu wengine, alionyesha kukerwa na kushindwa kuvumilia matendo ya wanyama hao alipokuwa jikoni katika nyumba anayoishi.
Kitu cha msingi anahitaji kuelimishwa na kupata ufahamu wa kutosha, ikiwamo kutambua kuwa wanyama hawana uwezo wa kiakili kama aliopewa binadamu. Vilevile wana haki ya kuishi na kutofanyiwa vitendo vya kikatili hata kama wamefanya baya kiasi gani. Jambo lingine la msingi ni kuheshimu na kutambua tamaduni na mitindo ya maisha ya tabaka zingine duniani ikiwamo zinazoamini haki za wanyama pengine kuliko za binadamu.
Tukio hilo pia limesababisha mitandaoni kuibuka na kila ukosoaji ikiwamo kukumbushiwa kwa tukio la kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson alikasika kiasi cha kubutua kiatu kilichopaa na kumpiga kichwani staa wa zamani wa klabu hiyo, David Beckham. Aliwakumbushia huu ulikuwa ni ukosaji pia, lakini tukio hilo halikushikiwa bango kama hili. Akahoji uhalali wa kutetea mnyama na kumuacha binadamu.
Haya yote yanaonyesha kuwa binadamu sio mkamilifu na anakosea, na anapobaini kukosea anapaswa kuomba msamaha. Ila kwa kumsaidia mkosaji ni vizuri akapewa ushauri na nasaha ambazo humpa ufahamu na kumfahamisha kosa ni lipi na nini anatakiwa kuepuka.
Mfano mzuri tumeshuhudia mchezaji wa Simba toka nchini Ghana, Bernard Morrison ambaye aliomba msamaha wiki iliyopita kwa kitendo cha kutoka kambini na kwenda mtaani. Na wiki hii klabu ya Simba ilitangaza kumsamehe na kumrudisha kambini kujiunga na wachezaji wenzake.

HILI NI FUNZO
Wachezaji ni vioo katika jamii na wanapaswa kuwa mfano mzuri wa kuigwa katika jamii siku zote kwenye maisha ya kila siku. Pale mchezaji anapokosea haraka anapotambua hilo ni muhimu kuomba msamaha kwa kile alichofanya.
Klabu zina jopo la madaktari, wataalamu wa saikolojia, walimu na viongozi. Hawa wanaweza kuwa washauri wazuri kwa mchezaji mkosaji hatimaye kumpa utulivu wa kiakili.
Kwa mchezaji ni kuhakikisha kosa alilofanya lisiwe la kujirudia kwani itaonyesha kuwa anafanya hivyo kwa makusudi. Mchezaji anapokosea asitengwe, bali apewe faraja na kuelimishwa kwa kosa alilofanya.
Ni katika mazingira hayo, binadamu yeyote anapoadhibiwa hapaswi adhabu kufikia mahala ikaanza kuwa tishio kwa maisha na afya yake.
Ieleweke kwamba, pale mtu anapojikuta katika mazingira ya kusakamwa sana huajikuta akiathirika kisaikolojia, jambo ambalo ni hatari zaidi kiafya kwani lina uhusiano na kuathiri mifumo muhimu ya utendaji wa mwili.