Zijue hisa, hatifungani na vipande.

tototundu

Kaka Mkubwa
Nov 26, 2021
23
21
6
1. Hisa ni nini?

Hisa ni sehemu ya umiliki wa kampuni. Hivyo hisa moja inawakilisha asilimia ndogo ya umiliki katika kampuni. Kama kampuni ina hisa milioni moja na mwekezaji anamiliki hisa 10,000, mwekezaji huyu anamiliki 1% ya kampuni. Mwekezaji anayenunua hisa basi ananunua haki ya kumiliki kampuni. Stahili za mwenye hisa ni pamoja na kushiriki katika kutoa maamuzi ya kampuni katika mkutano mkuu wa wanahisa na kupata gawio litokanalo na faida. Ana haki pia ya kuuza hisa zake kwa faida pale ambapo kuna ongezeko la thamani ya hisa.

2. Gawio ni nini?

Gawio ni malipo yanayofanywa na kampuni kwa wanahisa kutokana na faida ya kampuni. Malipo haya yanapendekezwa na wakurugenzi na kuidhinishwa na mkutano mkuu wa wanahisa. Gawio linaweza kulipwa kutokana na faida ya mwaka husika au malimbikizo ya faida za nyuma. Gawio linaweza kulipwa kwa fedha taslim au kwa kuwaongezea hisa wanahisa.

3. Hatifungani ni nini?

Hatifungani ni hati ya deni ambalo kampuni au serikali huwakopa wawekezaji kwa makubaliano maalumu na kuwalipa riba na marejesho baada ya kupevuka kwa hatifungani hiyo. Mwenye hatifungani anastahili kulipwa riba (kwa kawaida ni kila miezi sita) na kurudishiwa mtaji wake hatifungani ikishapevuka. Pale ambapo kampuni inafilisika, wanaomiliki hatifungani wana haki ya kulipwa pesa zao kabla ya wale wanaomiliki hisa.

4. Soko la hisa la Dar-es-Salaam ni nini?

Soko la Hisa ni soko ambalo huwezesha hisa, hatifungani na dhamana zingine zilizoorodheshwa katika soko hilo kuuzwa na kununuliwa. Bidhaa hizi huitwa dhamana au kwa lugha ya kigeni (securities). Soko la hisa hapa Tanzania limeanzishwa mwaka 1996 kama kampuni binafsi yenye dhima (limited by guarantee); kwa maana ya kwamba wanachama wa soko hawatakiwi kuweka mtaji wowote. Mwanzoni kulikuwa na wanachama 11 ambao ni madalali wa soko la hisa pamoja na wawekezaji wakubwa (Institutional investors). Soko la hisa lilianza kazi zake rasmi mwezi April mwaka 1998 wakati hisa za TOL Ltd zilipoorodheshwa na kuanza kuuzwa na kununuliwa. Soko la hisa ni soko ambalo linajiendesha lenyewe likisimamiwa na Baraza la Wadhamini (DSE Council).

5. Toleo la awali lina maana gani?

Toleo la awali ni mauzo ya hisa na dhamana kwa umma kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kukusanya mtaji. Kwa lugha nyingine inajulikana kama IPO (Initial Public Offer) Mauzo hayo yana kipindi chenye ukomo. Baada ya hapo, kama mwekezaji anataka kuwekeza kwenye kampuni hiyo atatakiwa kwenda kwenye soko la pili kupitia madalali wa soko la hisa.

6. Je kama nitanunua hisa ya kampuni halafu kampuni ikafilisika nitapataje fedha zangu?

Siku zote uwezekano wa kupata hasara au hatari za uwekezaji zinaendana na umiliki wa uwekezaji huo. Wamiliki wa hisa wanategemea kupata gawio pamoja na kupanda kwa bei ya hisa zao. Vivyo hivyo, kama kampuni itapata hasara basi idadi ya hisa zako zitabaki vilevile ila thamani itapungua. Na iwapo ikitokea kampuni ikafilisika kabisa basi sheria inaelekeza kuwa kutakuwa na mfilisi. Mfilisi kwanza kabisa anapaswa kulipa madeni kwa kutumia fedha za mauzo ya mali za kampuni, na kama fedha hizo zitabaki, watalipwa wanahisa wa kampuni hiyo. Endapo fedha hazitabaki, ni hasara kwa wenye hisa

7. Je ninapataje gawio langu?

Gawio ni faida ambayo analipwa mwanahisa iwapo kampuni imepata faida na kuamua kulipa sehemu ya faida kama gawio. Njia itumikayo kulipa inategemea na kampuni. Kampuni nyingi zinatumia Shirika la Posta pamoja na mabenki. Ni juu ya mwekezaji kuwasiliana na kampuni aliyowekeza na kutoa taarifa muhimu kama vile anwani ya posta pamoja na akaunti ya benki. Kama malipo yatalipwa kwa kupitia njia ya posta basi utapata Hawala ya Posta kupitia anwani yako, na kama malipo yanafanyika kupitia kwenye akaunti ya benki basi utapata hundi au pesa zitaingizwa kwenye akaunti yako. Ni muhimu kutoa taarifa iwapo anwani au akaunti yako itabadilika. Kampuni nyingi zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa zinatoa gawio mara mbili kwa mwaka.

8. Je ninaweza kuhamisha miliki ya hisa zangu kwa mke au mume wangu?

Ndiyo, hisa zinahamishika. Hisa zilizoorodheshwa Soko la Hisa la Dar-esSalaam zimehifadhiwa katika Hifadhi ya Dhamana, hivyo uhamishaji wa umiliki ni rahisi kuliko uhamishaji wa kutumia makaratasi na hati. Kwa kanuni za Soko la Hisa la Dar es Salaam, uhamishaji binafsi wa umiliki wa hisa huwezekana wakati dhamana haziko katika mnada. Hivyo uhamishaji wa umiliki wa hisa kutoka kwa mume kwenda kwa mke ni uhamishaji binafsi unaoruhusiwa.

9. Kuna tofauti gani kati ya Hisa na Kipande?

Hisa ni sehemu ya umiliki katika kampuni. Na kipande ni sehemu ya umiliki katika mfuko wa uwekezaji wa pamoja kwa maana ya Amana ya Kikundi (Unit Trust Scheme). Hisa ni sehemu ya umiliki wa kampuni fulani wakati kipande kinajumuisha mseto wa uwekezaji katika vitega uchumi mbali mbali.

10. Je thamani ya kipande inatafutwaje?

Thamani ya kipande (NAV) inatafutwa kwa kuchukua thamani ya mali zote za mfuko (rasilimali kwa maana ya kilichopo na kinachotegemewa kupokelewa) na kutoa madeni yanayotegemewa kulipwa, na gharama za uendeshaji na kugawanya kwa idadi ya vipande vyote vya mfuko.
 
  • Like
Reactions: Masika

Mkwavinyika

Administrator
Staff member
Dec 2, 2021
49
9
26
Dar es Salaam
Kuna hii post niliona mahali'

JE UNAELEWA NINI KUHUSU HISA?
Makampuni mengi yanayokuwa na mitaji mikubwa si kwamba huo mtaji wameupata wenyewe bali kuna michango midogo midogo ya watu wengine ambao wanaitwa wanahisa.Je hisa ni nini? Hisa ni kipande cha umiliki wa sehemu ya kampuni.Watu hualikwa kununua vipande hivyo katika kipindi Fulani inaweza kuwa wakati wa kuanzisha kampuni au baada ya kampuni kuanzishwa pale inapotaka kujipanua kimtaji na hasa inapo ingia katika soko la mitaji.
Vipande hivyo vinakua na thamani Fulani na unapo nunua kipande hata kimoja unakua na wewe kisheria unamiliki sehemu ya kampuni hiyo kwa kiasi cha thamani ya hisa ulizo nunua.Kwa mfano kama kipande kimoja ni sh 500 na ukanunua vipande 1000 tunasema umenunua hisa 1000 na utakua unamiliki hisa za shilingi laki tano 500 000 kwa muda huo.
Unaweza ukajiuliza je unafanikiwaje kupitia umiliki wa hisa katika kampuni? Ni swali zuri kujiuliza.Kila mwisho wa mwaka kunaitishwa mkutano mkuu wa wanahisa ambapo mambo mbalimbali hujadiliwa kuhusu kampuni husika mojawapo ya mabombo hayo ni kuhusu faida ambayo kampuni imepata na uamuzi kuhusu kuigawa au kuendelea kuiwekeza ili izae zaidi na zaidi.
Kama kampuni moja ya mipango yake ni kuendelea kuwekeza faida inayopatikana ili kampuni ikue haraka basi hapo swali la kila hisa kupewa gawio lake ndio linachukua nafasi.Kwa mfano kampuni itachua faida iliyopata baada ya kulipa madeni na kodi inayodaiwa na kugawanya kwa idadi ya hisa zilizopo na kupata faida kwa kila hisa na hapo ndipo kila mtu ataweza kujua faida aliyopata kwa kumiliki hisa katika kampuni.
Atajuaje? Ni rahisi tu.Atachukua idadi ya hisa anazomiliki na kuzidisha kwa kiasi cha faida kwa kila hisa iliyotangazwa na kampuni anayomiliki kihisa katika mkutano mkuu wa kampuni.Cha muhimu kufahamu hapa ni kwamba kiasi cha faida inayopatikana hutegemea jinsi kampuni itakavyofanya biashara yake katika mwaka husika na siyo kwamba gawio kwa kila hisa litakua halibadiliki.Linaweza kwenda chini au kupanda kutokana na mazingira ya kibiashara na sababu nyingine kiuchumi.
Kuna faida nyingi za umiliki wa hisa kwa mmiliki na kwa kampuni yenyewe.Kwa kampuni ni kwamba inakua na uhakika wa mtaji kuendelea kubaki kwa muda mrefu kwa sababu hata mtu akiamua kuuza hisa zake nafasi itabaki pale pale maana zitanunuliwa na mtu mwingine ambayo ni faida pia kwa mmiliki pale anapoona kuwa hana huitaji wa kumiliki hizo hisa katika hiyo kampuni kwa muda huo.s
Ni faida pia kwa kampuni kutoa fursa ya hisa kuliko kwenda kukopa kwenye taasisi za kifedha.ili taasisi ya kifedha ikopeshe kampuni ni lazima kampuni hiyo isiwe na madeni mengi ili uwezekono wa kulipa uwe mkubwa.Na hisa hazijumuishwi kwenye idadi ya madeni ya kampuni kama ilivyo mikopo.Hivyo basi kampuni zinazotoa hisa huwa na nafasi kubwa ya kwenda kukopa na kukuza mtaji wake.
AINA HISA NAZO NI
1. HISA ZA WAMILIKI
Hizi ni aina za hisa ambazo huwa ndio nyingi katika kampuni. Wale wanaomiliki hisa nyingi katika kampuni hisa zao huitwa hisa za wamiliki. Huitwa hisa za wamiliki kwakuwa hawa huhesabika kama ndio kampuni yenyewe na hivyo wenye hisa hizo ndio wamiliki wa kampuni. Nimesema hapo juu kuwa wanahisa hawana haki sawa, wajibu pamoja na uwajibikaji. Wenye hisa hizi wana haki kubwa ya kimaamuzi katika shughuli zote za uendeshaji wa kampuni kwakuwa wao kila hisa moja huwa ni kura moja na kwahiyo kila kitu hupitishwa kwa kura zao. Pia wana haki ya kupata mgao mkubwa kuliko wengine. Hata hivyo wanawajibika zaidi linapotokea tatizo kwa mfano inapotokea hasara wao ndio hupoteza zaidi. Kwa jina jingine hisa za hawa huitwa HISA ZA SIMBA( LIONS SHARE). Hii ni kwasababu huko mwituni simba hupata mgao mkubwa wa nyama kati ya wanyama wote.
2. HISA ZA KAWAIDA.
Hizi ni zile hisa ambazo humilikiwa na watu wengine wa kawaida katika kampuni. Mara nyingi hawa ndio huwa wengi japo kila mtu huwa na hisa kidogo kidogo. Mgao wao wa faida hutokana na asilimia ya kile mtu anachomiliki. Maamuzi yao katika kampuni huwa ni madogo ukilinganisha na wenye zile hisa za umiliki( equity shares). Hata hivyo uwajibikaji wao nao ni mdogo pia kwani hupata hasara kidogo pale kampuni inapopata hasara. Pamoja na hayo sheria imewapa kipaumbele cha kupewa mgao wa faida kabla ya kundi jingine lolote.
3. HISA ZA WAANZILISHI
Hizi ni hisa ambazo hutolewa kama zawadi kwa waanzilishi wa kampuni. Mgao wa faida wa hisa hizi huwa sio wa moja kwa moja isipokuwa hutegemea na faida inayozidi. Kawaida mgao wa faida kwa wanahisa wengine hutoka katika faida ya kawaida lakini hawa hawapewi mgao kutoka faida ya kawaida isipokuwa hupata pale faida inapozidi au kuvuka kiwango ilichotegemewa.
4. HISA ZA KAMPUNI
Zote nilizotaja juu ni hisa za kampuni lakini bado jina hili hupewa hisa hizi kutokana na kuwa ni hisa maalum ambazo hutolewa kwa waajiriwa/wafanyakazi katika kampuni husika. Waajiriwa hutengewa hisa zao na mwenye uwezo huweza kuchukua hisa hizo kwa kiwango cha uwezo wake. Mwajiriwa huendelea kuwa na hisa hizo hata baada ya utumishi wake kukoma . Kwa ufupi sana niseme tu kuwa hisa sio hisa ila hisa ni una hisa za aina gani.
 
  • Like
Reactions: Masika