Keane abadili mkeka, asema Arsenal Top 4
LONDON ENGLAND. ROY Keane ameamua kubadilisha utabiri wake wa Top Four na kusema sasa Arsenal itaibwaga Manchester United kwenye mbio za kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Manchester City, Liverpool na Chelsea zikiwa zimejiweka pazuri kwenye nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, nafasi moja iliyobaki kwenye kutoa tiketi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inashindanisha timu za Arsenal, Man United na Tottenham.
Man United ilionekana ipo pazuri wakati iliposhinda 4-2 dhidi ya Leeds United, lakini matokeo ya hovyo yalifuatia ikiwamo sare na Watford kisha kichapo cha Manchester City kimevuruga kabisa mipango na kuporomoka hadi kwenye nafasi ya tano, huku Arsenal wakishinda mechi yao ya Watford mabao 3-2 juzi Jumapili. Arsenal yenyewe imeshinda mechi tatu mfululizo.
Keane aliamini kwamba Man United itafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya ushindi ule wa Elland Road, lakini sasa amebadili utabiri wake, akisema: “Nadhani Man United kushika namna nne itakuwa nzuri kwao. Kumekuwa na kelele nyingi za wachezaji kutaka kuondoka, mikataba yao ikiwa dhida kama Pogba na Jesse Lingard. Mtazamo wa Man United kwa miezi michache ijayo ni kujaribu kuikamatia nafasi nne.
“Wana mechi ngumu ya Ulaya inafuata, wanapaswa kujikusanya na kuwekeza akili kwenye hilo jambo, watakuwa sawa.”
Hata hivyo, kiungo huyo wa zamani wa Man United amebadili mawazo, akisema Arsenal wana nafasi kubwa ya kumaliza Top Four. Keane alikoshwa na ushindi wa Arsenal dhidi ya Wolves uwanjani Emirates na kusema Arsenal ya sasa si timu laini tena.