He! Eti Messi chanzo Mbappe kuondoka

PARIS, UFARANSA. USAJILI wa supastaa Lionel Messi huko Paris Saint-Germain umeripotiwa kuchochea uamuzi wa Kylian Mbappe kutaka kuachana na miamba hiyo ya Ligue 1, ripoti kutoka Ufaransa zimeeleza.
Bao la dakika za majeruhi la Mbappe lilifanya PSG kupata ushindi muhimu dhidi ya Real Madrid kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne iliyopita, ambapo Messi alikosa penalti baada ya kipa Thibaut Courtois kuokoa.
Straika, Mbappe mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu huu huko Parc des Princes na kumekuwa na ripoti kwamba ataelekea zake Bernabeu. Hata hivyo, ripoti nyingine inadai kwamba PSG imepanga kumfanya Mbappe kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa ili alingane na masupastaa wengine kwenye kikosi hicho ni Messi na Neymar.
Na sasa akiwa amebakiza miezi minne ya mkataba wake huko Parc des Princes kumekuwa na maelezo kwamba mchezaji huyo anaweza kuondoka bure kwenda Los Blancos kama hakutakuwa na jitihada kubwa za PSG katika kumbakiza.
Kinachoelezwa ni kwamba uamuzi wa klabu kumchukua Messi kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi limetibua hali ya mambo kwenye vyumba vya kubadilishia vya klabu hiyo, ambapo amevunja ule uhusiano matata kwenye fowadi sambamba kati ya Mbappe na Neymar. Messi kwa sasa amekuwa na sauti kubwa huko kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kutokana na hadhi yake kwa wachezaji wengine.
Mbappe amefunga mabao 22 na kuasisti mara 16 msimu huu, akitengenezea nafasi ya kuwa staa muhimu kabisa kwenye kikosi hicho cha kocha Mauricio Pochettino na hakika bila ya mabao yake, timu hiyo ingekuwa inapata shida kushinda mechi zake.