Mavitu ya Saka, Odegaard yampagawisha Fabregas
LONDON ENGLAND. NAHODHA wa zamani wa Arsenal, kiungo fundi wa mpira wa Kihispaniola, Cesc Fabregas amesema Bukayo Saka na Martin Odegaard ndiyo silaha ya sasa na ya baadaye ya wababe hao wa Emirates baada ya kile walichowafanya Watford kwenye mchezo wa Ligi Kuu England juzi Jumapili.
Odegaard alifunga bao la kuongoza la Arsenal uwanjani Vicarage Road, kisha Saka na Gabriel Martinelli nao kila mmoja walitikisa nyavu kwenye ushindi wa 3-2 na kuwaporomosha Manchester United kwenye Top Four kabla hata hawajachapwa na mahasimu wao Manchester City.
Saka alifunga bao lake la tisa kwenye klabu hiyo msimu huu, wakati Odegaard amefunga bao lake la tano tangu alipojiunga akitokea Real Madrid.
Kwa Saka, bao hilo la Vicarage Road linampeleka kwenye nafasi nzuri ya kufikia rekodi ya Fabregas kwenye klabu hiyo.
Kwa ujumla wake, Saka amefunga mabao 20 akiwa na uzo wa Arsenal, huku akiwa na umri wa miaka 20, hivyo staa huyo Mwingereza anakuwa mchezaji mwenye umri mdogo kufikisha idadi hiyo ya mabao kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15 kupita. Saka amefikisha akiwa na umri wa miaka 20 na siku 182.
Fabregas alisema: “Saka na Odegaard ni silaha ya sasa na baadaye Arsenal. Vipaji viwili vikubwa kabisa,” alisema kiungo huyo wa Monaco, ambaye alifunga mabao 57 kwenye kikosi hicho.
Kabla ya mechi hiyo ya Watford, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alimsifu Odegaard akisema kiungo huyo atafunga mabao mengi sana.
“Martin kwetu sisi ni mchezaji muhimu sana amekuwa akionyesha hilo kila wiki,” alisema Arteta.
“Anapiga kazi kwenykweli, amekuza kiwango cha mpira wake kama tulivyojadili na kukubaliana. Amejiandaa vyema kiakili kwa namna anavyocheza.”