Neville adai anawajua wanaotibua Man United.
MANCHESTER, ENGLAND. KIMENUKA. Gary Neville amesema anawajua mastaa wa Manchester United wanaotibua mambo kwenye vyumba vya kubadilishia vya klabu hiyo na kufanya timu kupata matokeo ya hovyo uwanjani.
Upo ushahidi wa kutosha kwamba kuna utovu wa nidhamu mkubwa ndani ya kikosi hicho cha kocha Ralf Rangnick, ambapo mastaa wa Man United wamefikia hatua ya kumpachika jina la hovyo kocha msaidizi, Chris Armas wakifanya dhihaka.
Rangnick yupo kibaruani Man United kama kocha wa mpito kwa zaidi ya miezi miwili sasa, huku timu yake ikipata matokeo yasiyoeleweka na kuelezwa hali si nzuri kwenye vyumba vya kubadilishia.
Ripoti za mapema Januari zilizotolewa na Mirror Football, zilifichua kwamba wachezaji wa Man United wanabeza mbinu za ufundishaji za Rangnick kwamba zimepitwa na wakati na haziwezi kusaidia kitu kwenye Ligi Kuu England. Tatizo jingine kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ni ripoti ya wachezaji wanamtaka kocha wa Paris Saint-Germain, Mauricio Pochettino apewe mikoba ya kuinoa timu hiyo mwishoni mwa msimu huu na sio kumpa ajira ya moja kwa moja Rangnick.
Nahodha na beki wa zamani wa Man United, Neville amewachurukia wachezaji ambao wanapiga kampeni ya kuchafua hali ya hewa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Beki wa kulia huyo wa zamani huko Old Trafford alisema: “Ile Ijumaa kulifanyika utovu mkubwa wa nidhamu, sikupenda. Walikuwa wakimwita msaidizi namba mbili wa Ralf Rangnick jina la Ted Lasso, haukuwa utani, huo ni utovu wa nidhamu, sikupenda kabisa.
“Ile nadhani imefichua kila kitu kuhusu wao, hawana heshima. Nadhami kama ningekuwa Ralf Rangnick na msaidizi wake ningekuwa tofauti na nisingetaka kuendelea kuwa sehemu ya timu hii yenye maneno maneno ya kijinga. Hilo haliwapo kipindi chetu.
“Nakumbuka mwanzoni wakati najiunga na Sky na kulikuwa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo nilikwenda Napoli kwenye mechi dhidi ya Chelsea. Ilikuwa mechi ambayo Andre Villas-Boas aliwaweka benchi Frank Lampard, Michael Essien, Ashley Cole mastaa wanne au watano muhimu kwenye kikosi. Baada ya hapo kila kitu kilitibuka.
“Mambo yalikwenda haraka sana kwenye vyombo vya habari, taarifa zilivuja. Tukasikia kocha anafukuzwa. Nikajiuliza hivi vitu vinatokea kweli? Mawakala wa wachezaji ndio walikuwa wakiviambia vyombo vya habari kilichokuwa kinaendelea ndani ya Chelsea.
“Hicho ndicho kinachoendelea Manchester United kwa sasa.
Hali ya mambo kwenye kikosi cha Man United sio nzuri. Supastaa Cristiano Ronaldo ameambiwa aende kujiunga na Bournemouth kwa sababu yeye ni sehemu ya tatizo la kinachoendelea kwenye kikosi hicho cha Old Trafford. Baada ya sare dhidi ya Southampton Jumamosi iliyopita, Man United inakabiliwa na vita kali kwenye harakati zao za kumaliza ndani ya Top Four msimu huu.
Ronaldo alirudi Man United kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi na ndiye kinara wa mabao, akiwa amefunga mara 14.
Lakini, sasa amecheza mechi sita bila ya kufunga na hilo limeibua maswali kama bado ana uwezo wa kuchezea timu kubwa.
Tetesi zinasema amemwambia wakala wake Jorge Mendes amtafutie timu ili aachane na Man United mwisho wa msimu.
Na sasa mtangazaji wa zamani wa Sky Sports, Richard Keys ameiambia beIN Sports, Ronaldo anapaswa kuuzwa haraka.
Alisema: “Jorge Mendes amezungumza na mabosi wa Man United kuhusu kuondoka mwisho wa msimu. Kwa maoni yangu, anapaswa aondolewe haraka. Nimekuwa nikisema karibu msimu wote, nadhani yeye ni sehemu ya matatizo, sio tatizo la timu nzima, hakuna mwingine.”
Mtangazaji mwingine, Andy Gray alisema: “Umri wake ni miaka 37. Kama anataka kucheza kila mechi, aende akasajiliwe Bournemouth huko atacheza kila wiki.”