Kotei ashushwa Dar usiku mnene.
HII inaweza kuwashtua mashabiki wa Simba, ila ndio ukweli ulivyo klabu ya DTB, vinara wa Ligi ya Championship ni balaa baada ya kumshusha usiku mnene kiungo wa zamani wa Msimbazi, James Kotei kisha kumpa mkataba wa miaka miwili fasta ili kuichezea timu yao.
Nyota huyo aliyeitumikia Simba kwa misimu kama mitatu tangu 2016 hadi 2019 kisha kutimkia Sohar SC ya Oman ambako baada ya kuvunja mkataba wake sasa amerejeshwa nchini lakini sio kukipiga tena Msimbazi ila kwa DTB inayozidi kutisha kwenye Championship.
Mmoja wa viongozi wa juu wa DTB ambaye hakutaka jina lake kutajwa aliliambia Mwanaspoti kuwa kiungo huyo atatambulishwa rasmi Januari 15, ambayo ni siku ya mwisho ya dirisha dogo la usajili kufungwa.
“Ni kweli Kotei tupo naye hapa nchini kwa mapendekezo ya kocha Ramadhan Nswanzurimo na tulitarajia kumtangaza kama sapraizi kwenye mchezo wetu na Kitayosce Januari 15,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mbali na usajili wa Kotei ila DTB imenasa saini ya beki wa kushoto raia wa Uganda, Shafik Batambuze kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Kabwe Warriors ya Zambia kufuatia kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja.
Licha ya kutoweka wazi taarifa hizo, mratibu wa timu hiyo Muhibu Kanu alisema kuwa wachezaji bora watasajiliwa kwa mapendekezo ya Kocha Mkuu kwani malengo yao ni kucheza Ligi Kuu Bara.