YANGA YAIZIMA AZAM CHAMAZI, YAIPIGA 2-1
VIGOGO, Yanga SC wamepiga hatua kubwa katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Azam FC usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Haukuwa ushindi mwepesi, kwani ilibidi Yanga watoke nyuma baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema na Azam FC lililofungwa na mshambuliaji Mzambia, Rodgers Kola dakika ya 11.
Iliwachukua dakika sita tu Yanga kusawazisha bao hilo, mfungaji beki Mkongo Djuma Shabani kwa penalti kufuatia kipa Ahmed Ali Suleiman Salula kumdaka miguu kiungo Mrundi, Saido Ntibanzokiza akiwa anakwenda kufunga.
Na kinara wa mabao wa Yanga, Mkongo mwingine, Fiston Kalala Mayele akaifungia timu hiyo bao la ushindi dakika ya 78 akimalizia krosi ya Djuma Shabani, mchezaji mwenzake wa zamani wa AS Vita ya kwao, Kinshasa.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 51 katika mchezo wa 19 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi 14 zaidi ya mabingwa wa zamani, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi.
Azam FC inabaki na pointi zake 28 za mechi 19 sasa katika nafasi ya tatu.