Shikalo azungumzia Yanga, Dube amliza
UKIANZA kutaja majina ya makipa ambao walikuwa na wakati mzuri ndani ya Yanga huwezi kuacha kulitaja jina la Faruk Shikhalo ambaye alicheza kwenye kikosi hicho kwa misimu miwili mfululizo akitafuta ugali wake na maisha mengine yaendelee.
Shikhalo aliondoka mwishoni mno kwenye kikosi hicho na kusajiliwa, Diara Djigui na kuwafanya mashabiki wengi wajiulize namna alivyoachana na timu hiyo huku wengi wao wakitarajia kuona akiendelea kuitumikia Yanga kwa msimu wa tatu.
Kwasasa kipa huyo yupo katika kikosi cha KMC akiendelea kufanya yake licha ya kukutana na ugumu wa namba mbele ya mkongwe, Juma Kaseja ana uhakika wa kucheza kutokana na uwepo wake kwa misimu mitatu mfululizo pamoja na unahodha.
Mwanaspoti lilimfuata Shikhalo hadi kambi ya timu yao iliyopo Bunju A na kupiga naye stori nyingi juu ya namna ambavyo aliondoka kwenye kikosi cha Yanga, maisha ambayo aliishi katika timu hiyo na malengo yake ya sasa akiwa KMC.
MISIMU MITATU MICHUNGU
Shikhalo anasema kwenye misimu yake mitatu ambayo amecheza Tanzania hawezi kusema alikuwa kwenye urahisi bali alikumbana na ugumu mkubwa wa kuzoea mazingira kwa uharaka kwa sababu upande wa Ligi ya Tanzania hakuna utofauti mkubwa.
Kipa huyo anasema kucheza Tanzania lazima ujue utamaduni ili upate nafasi, pia ilikuwa ni ngumu kujua viwanja bora na timu nzuri, lakini kwasasa anajua kila kitu kutokana na kukaa kwa muda mrefu nchini.
“Safari yangu haikuwa nzuri wala mbaya sana naweza kusema hivyo, kiukweli kwasasa najua viwanja vyote lakini awali ilikuwa ngumu, kwasasa najua hata Tanzania Prisons mshambuliaji fulani hatari kwahiyo inanisaidia kupambana uwanjani,” anasema na kuongeza;
“Tanzania mpira ni mgumu sababu kuna mazingaombwe mengi kwenye maisha ya mpira, ukikaa kawaida na wenzako kuna vitu unajifunza na kujionea kwenye ‘stori’, kikubwa namshukuru Mungu kwa kunisimamia mpaka leo naendelea kuwa Tanzania nikiwa naenda mwaka wa tatu.”
YEYE NA MNATA FRESHI TU
Kama unazani makipa Metacha Mnata na Shikhalo walikuwa kwenye sintofahamu wakati wanaitumkia Yanga basi unajidanganya kwa sababu majamaa hao walikuwa wanashirikiana vya kutosha kuhakikisha timu yao inashinda na kujiweka sehemu nzuri.
Shikhalo anasema anamshukuru sana Mnata kwa misimu miwili waliyokuwa wote kwa sababu walipitia kwenye wakati mgumu na mzuri na hayo yote yalikuwa katika harakati za kuipambania timu yao ipate ushindi kwenye mechi zao.
“Mnata ni mtu ambaye tulipeana changamoto vizuri sana bila kumsahau Kabwili (Ramadhan) alikuwa akitusapoti, changamoto kwenye timu kubwa ni kawaida kwa sababu kuna muda yapo mabaya na muda mwingine unapitia mazuri,” anasema na kuongeza;
“Yanga ni timu kubwa na namshukuru mwenyezi Mungu nimecheza kwenye kiwango kikubwa, presha yake imenijenga kwa sababu unapozungumzia kuhusu mchezaji mzuri basi ni yule ambaye anaweza kuendana kwenye mazingira ya kucheza kwa presha.”
Shikhalo anaongeza na kusema;”Kabwili naye sio kipa mbaya ni mzuri na kwa baadaye atakuja kuwa kipa mzuri kama ataendelea.”
DUBE AMLIZA
Shikhalo anasema kwa misimu yote miwili ambayo amecheza Tanzania akiwa na Yanga hawezi kusahau kabisa bao alilofungwa na mshambuliaji wa Azam, Prince Dube Aprili 25, 2021 kwani lilimfanya amwage chozi uwanjani baada ya kuona amewaangusha wenzake.
Yanga kwenye mchezo huo ilifungwa 1-0 na mchezo ulimalizika Azam ikiibuka na ushindi huku wakiweka pointi tatu mfukoni.
“Nilijihisi kabisa nimewaangusha wenzangu kwa sababu tulipambana sana licha ya kukosa mabao mengi, kwa muda ule kuruhusu bao dah sikuwa poa, hakuna mtu ambaye anapenda kuwaangusha wenzake na nashukuru Mungu baada ya mchezo wenzangu waliniambia imeshaisha maana huu mpira leo kwangu kesho kwao,” anasema na kuongeza;
“Nashukuru Mungu upande wa mashabiki sikuwahi kuwa nao kwenye shida kabisa, muda wote ambao nimekuwa nao Yanga wa miaka miwili sikuwahi kuwa nao kwenye shida kabisa kiukweli nisiwe muongo na nashukuru kwa hilo.
BOCCO AMTESA DERBY
Shikhalo anasema kila wakati wanakuwa wanakutana na mechi ya watani wa jadi mtu ambaye alikuwa anamfikilia ni mshambuliaji wa Simba, John Bocco kwa sababu hakuwahi kabisa kukutana naye lakini baada ya kucheza naye mechi mbili basi alimjua vizuri.
Kipa huyo anasema Bocco ni mzuri sana kwenye mipira ya vichwa na sizani kama ana udhaifu bali kwenye upande niliokuambia basi ni hatari zaidi na hiyo ipo hata sisi kwetu makipa yupo ambaye anaweza kucheza uso kwa uso na mwingine anacheza mbali, mwingine krosi.
“Upande wa kina Kagere, Kahata nilishacheza nao Kenya lakini tofauti na Bocco, yeye pia baada ya kukutana naye mara mbili nilimjua vizuri, mimi nimecheza mechi nne za debi na Metacha nne kati ya nane kwahiyo nilimsoma vizuri.”
KOMBE LAMUUMIZA
Hapa Shikhalo anainama kisha anainuka na kusema licha ya kucheza misimu miwili Yanga na kumaliza nafasi ya pili hawezi kujipiga kifua kwa sababu hajafanikiwa kabisa kutoka na kombe la Ligi Kuu kwa sababu yalikuwa malengo yake yeye mwenyewe wakati anasajiliwa na Yanga.
Shikhalo anasema kama mchezaji alikuwa anatamani abebe ubingwa na Yanga lakini jambo hilo halijafanikiwa na baadaye alijitahidi kuhakikisha anawapa furaha mashabiki wa Yanga kwa kuwapa ubingwa wa Kombe la Mapinduzina alifanikiwa.
“Tulibeba ubingwa wa Mapinduzi na nilikuwa kipa bora, hivyo sikuwaacha watupu kabisa, mashabiki walikuwa na furaha kisha matunda niliyaona baada ya kupewa shilingi kadhaa na wao baada ya kuona nimewapa kitu fulani, nashukuru sana.”
Hali ya kukosa ubingwa inawatesa mpaka sasa mabosi wa Yanga wanahangaika kuhakikisha wanapata kombe msimu huu mbele ya Simba ambao wameanza ligi kwa kusua sua.
AACHWA MATAA YANGA
Shikhalo anapatwa na kigugumizi alipoulizwa namna ambavyo aliondoka Yanga, kipa huyo aliinama kisha anasema; “Kutokana na kufanya vizuri kwangu nikiwa na Yanga kiukweli sikutarajia kabisa kama naweza kuondoka Yanga na nilikuwa na ubora wakati mkataba wangu unaenda kuisha.”
Kipa huyo anafunguka zaidi na kusema kocha Nasreddine Nabi tayari alikuwa na pendekezo lake la Diara (Djigui) na mkubwa siku zote hakosei hivyo aliheshimu uamuzi wa kocha na kutakiana naye kheri kwa sababu mpira ni mchezo wa kuonana.
“Nilikuwa nasubili lolote ujue maana mkataba wangu ulikuwa unaenda ukingoni, tulivyomaliza msimu niliondoka kwenda nyumbani kwa ajili ya mapumziko na suala langu lipo kwa kocha lakini siku chache CECAFA ilipokuwa inaendelea Rama (Kabwili) alipata kadi nyekundu na mwalimu aliniomba nirudi,” anasema Shikhalo na kuongeza;
“Niliporudi nilicheza mechi moja wakataka niendelee kucheza lakini mimi nikawaambia hapana nitakuwa simtendei haki Kabwili kwa sababu yeye alikuwa ameshaanza, basi mwenzangu aliendelea na bahati mbaya tukatolewa kwenye mashindano.”
Shikhalo anaongeza na kusema; “Baada ya kama wiki akatambulishwa Diara huku mimi nikiwa sijaambiwa lolote lile, baadaye nikaitwa ofisini viongozi wakaniambia mwalimu amemtaka waliomsajili basi nikachukua mizigo yangu, nilipokea vizuri kwa sababu kwenye mpira huwa inatokea.”
APATA OFA NJE, DANTE AMVUTA KMC
Kipa huyo baada ya kuchukua mabegi yake na kuondoka Tanzania anasema alipata ofa tatu kutoka nchi ya Ethiopia na Zambia lakini alipoziangalia aliona Ligi ya Ethiopia ipo chini na upande wa Zambia kwenye kipengele cha pesa hawakuwa vizuri.
Wakati akiwa anazidi kuchang anua alipokea simu kutoka kwa bosi wa KMC na yeye aliangalia ubora wa Ligi pamoja na ofa akaona bora arejee nchini Tanzania kwa ajili ya kucheza na kuendelea kuonekana kama ilivyokuwa wakati anacheza Yanga.
“Unajua hata kama unapokea kidogo hapa lakini ligi ni nzuri na inafatiliwa na watu wengi, baada ya kupigiwa simu na kiongozi wa KMC basi nilikata simu na moja kwa moja nilimtafuta Dante (Andrew Vicent) nikamuuliza kuhusu timu na suala zima namna ambavyo inaenda, alinielelezea na mimi nikasema basi naweza.”
Shikhalo anasema baada ya kutua KMC haoni tofauti yoyote kutokana na yeye ni mtu wa watu hivyo anachukulia maisha kama kawaida na hakuna tofauti yoyote ile ambayo anakutana nayo isipokuwa mashabiki mtaani wanapokuona lazima waanze kukushangaa.
“Mtaani kidogo ilitaka kuwa changamoto lakini uzuri ni kwamba hawakuzungumzii kwa ubaya, upande wa wachezaji Dante alinipokea vizuri sana na niliwahi kufanya naye kazi kwa mwaka mmoja Yanga, nashukuru Mungu naendelea vizuri.”
HAJAKATA TAMAA
Shikhalo baada ya kuingia KMC alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kupoteza mechi kadhaa na baadhi ya mashabiki wakiona kama vile tayari ameshapoteza muelekeo lakini mwenyewe anasema yeye hakuwahi kukata tamaa na ndio maana timu yao imerejea kwenye mstari kidogo kidogo. “Nashukuru kwanza kwa uzoefu wangu mdogo wa miaka 10 kucheza Ligi Kuu imenisaidia kujua kuna nyakati ngumu na nyepesi kwenye mpira, kikubwa ni kuendelea kuweka bidii na kuomba sana kwa Mungu ili azidi kunifanyia wepesi kwenye kazi yangu,” anasema Shikhalo.
Kipa huyo anasema yapo magoli ambayo amefungwa na anayajutia lakini siku zote yeye ana amini kipa mazuri anafungwa mabao ya ajabu kwa sababu mabao magumu lazima ahakikishe anayacheza na hiyo sio kwake bali ni kwa makipa wote.