MJUAJI: Kisa cha Yanga kupasuka 1976
WAJUAJI tu ndio tunaolijua hili. Klabu ya Young Africans (Yanga) ilipasuka vipande viwili 1976.
Kisa na mkasa kilianza 1968. Mwaka huo Mwenyekiti wa Yanga, Kondo Kipwata alimwachia uongozi kwa hiari Mwenyekiti mpya, Mangala Tabu.
Sababu ya kumwachia. Alikuwa akitakiwa mtu msomi wa kuisimamia klabu na hata kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa jengo lake. Katika makubaliano ambayo hayakuwa rasmi, ilikubaliwa baada ya kukamilisha ujenzi Mangala arudishe uongozi wa klabu kwa Kipwata. Lakini mambo yalienda ndivyo sivyo. Hata baada ya kukamilisha ujenzi, Mangala alisimama imara na aliandaa mkutano ili kujisimika rasmi katika himaya hiyo ya Jangwani.
Wapinzani wake wakiongozwa na Kipwata na Mwambungu hawakukubali. Mgogoro ukaanza chinichini tangu 1975 japo mambo yalikuwa chinichini mwaka huo ndio Nyota Afrika ilibeba ubingwa.
Licha ya mgogoro kufukuta, Yanga ilienda kubeba ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup). Katika fainali hizo za 1975, Yanga iliitungua Simba kwa mabao 2-0 na mwaka uliofuata Yanga ilikuwa inaenda Mombasa kutetea taji, tayari mgogoro ukiwa umekolea baada ya Kocha Tambwe Leya kuwashutumu baadhi ya nyota wake kuwa wanaihujumu timu hiyo.
Hii ni baada ya matokeo ya mchezo wa Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) kati yao na Enugu Rangers, Yanga ikitolewa kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka suluhu ugenini na sare ya 1-1 nyumbani.
Kabla ya kuondoka kwenda Mombasa, Tambwe alitaka kuwakata wachezaji wawili Sunday Manara na Gibson Sembuli, lakini uongozi wa Mangala ulipinga na kuwarudisha kundini. Katika michuano hiyo ya 1976, Yanga ilienda Mombasa na kufika fainali.
Hata hivyo, ilifika fainali na kukosa ubingwa mbele ya Luo Union ya Kenya kwa kufungwa 2-1. Huku nyumbani kulifanyika mkutano mkuu katika jengo la klabu hiyo na kina Mwambungu walimng’oa Mangala. Katika vurugu zilizotokea Mangala alitoroka klabuni kwa kuvaa baibui kupitia mlango wa nyuma kutokea Mtaa wa Nyati na Kongo na kutokomea zake.
Yanga ilibaki na wachezaji sita tu
Wachezaji wa Yanga walipotua Uwanja wa Ndege wa jijini Dar es Salaam (JNIA) walikutana na viongozi wa pande mbili. Wote wakiwa na usafiri wa mabasi ya kuwapokea. Upande mmoja alikuwa Mangala na mfadhili wa zamani wa Yanga, Shiraz Shariff na mwingine ulikuwa na Mwambungu na baadhi ya viongozi waliokuwa wakimsapoti Kipwata.
Wachezaji walitakiwa kuchagua basi la kupanda, huku viongozi hao wakitoa maneno ya ushawishi ili wapande mabasi yao. Ndipo Yanga ilipobakiwa na wachezaji sita tu. Wachezaji hao walikuwa ni Mwinda Ramadhani (Maajabu), Ahmed Omary na Juma Shaaban. Wengine ni Patrick Nyaga, Gibson Sembuli na Suleiman Said Sanga.
Wachezaji wengine wote waliondoka na Mangala ambaye alikuwa amepanga kuanzisha timu mpya. Hata hivyo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lilipinga kuanzishwa kwa timu mpya kipindi hicho.
Ilibidi wachezaji waliobaki wote wapelekwe Nyota Afrika ya Morogoro. Wachezaji walienda upande wa pili ni Athuman Mambosasa (aliyekuwa amejiunga Yanga akitokea Simba), Boi Idd ‘Wickens’, Leodegar Chilla Tenga, Jella Mtagwa, Kitwana Manara, Sunday Manara na Hassan Gobosi. Baadaye Juma Shaaban na Patrick Nyaga nao walirudi na kujiunga na wenzao Mseto ambayo pamoja na kuwa timu ya Morogoro, lakini ilikuwa ikifanya mazoezi Jangwani, Dar es Salaam.
Pan Africans yaanzishwa
Wachezaji wengine waliokuwa Yanga walikataa kujiunga na Nyota Afrika pamoja na kuwa upande wa Mangala. Hao ni waliotokea Yanga Kids na kupandishwa timu kubwa. Wachezaji hao ni Juma Pondamali, Jaffar Abdulrahaman na Mohammed Rishard ‘Adolf’. Wengine ni Mohammed Yahya ‘Tostao’, Kassim Manara, Said Mmanga, Ziara Mkuya, Sululu na Godwin Mapango. Hawa waliamua kujiunga na Klabu ya Breweries ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu wachezaji hao walijiunga na wenzao wa zamani waliounda Mseto ya Morogoro na kuanzisha Pan Africans. Kwa kuwa kulikataliwa kuanzishwa timu mpya, upande wa kina Mangala walifanya ujanja na kujiunga na timu moja iliyokuwa na masikani Upanga jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo iliyokuwa ya wachezaji wakongwe kufanya mazoezi ya kupunguza vitambi ilikuwa imesajiliwa kwa jina la Zama za Kale. Viongozi wa timu hiyo na wale wa Yanga zamani walikubaliana kufanya uchaguzi na wote kuiongoza timu hiyo ambayo waliibadili jina na kuiita Pan Africans. Jina likishabihiana na Harakati za Mapinduzi barani Afrika. Timu hii ilileta chachu kubwa ya upinzani kati yake na Yanga na hata kwa Simba. Nayo ilikuwa na masikani yake Mtaa wa Swahili na Mkunguni, Kariakoo jijini Dar es Salam ilipokaribishwa na Bendi ya Taarabu ya Egyption.
Baadaye timu hiyo ilihamia Mtaa wa Swahili na Amani, Kariakoo yalipo masikani hadi sasa na kwa jinsi ilivyoendeshwa kitajiri Pan ilitwaa ubingwa wa Bara 1982. Sio kubeba ubingwa, lakini ilisumbua nchini na kuvitoa jasho baadhi ya vigogo vya Afrika ikiwamo AS Vita ya DR Congo.
Kwa sasa timu hiyo inashiriki Ligi ya Championship ikiwa imeshasota sana ligi za madaraja ya chini kiasi cha kukimbilia kununua baadhi ya timu ili irejee Ligi Kuu bila mafanikio. Nawe sasa umeshakuwa mjuaji.