IVORY COAST, MALI NA GAMBIA ZASHINDA 1-0 AFCON.
TIMU ya taifa ya Ivory Coast imeanza vyema Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Equatorial Guinea usiku wa Jumatano bao pekee la kiungo wa Sivasspor ya Uturuki, Max-Alain Gradel dakika ya tano katika mchezo wa Kundi E Uwanja wa Douala Jijini Douala, Cameroon.
Nayo Gambia imeichapa Mauritania 1-0, bao pekee la kiungo wa RFC Seraing ya Ubelgiji, Abdoulie Jallow mchezo wa Kundi F Uwanja wa Limbe Jijini Limbe.
Mechi nyingine ya Jumatano, bao pekee la mshambuliaji wa Sarpsborg 08 ya Norway, Ibrahima Koné kwa penalti dakika ya 48 limeipa Mali ushindi wa 1-0 dhidi ya Tunisia katika mchezo wa Kundi F hapo hapo Limbe.