Wachezaji Wote Ligi Kuu Bara Watolewa AFCON.
Kuanzia Januari 9, 2022, mashabiki wa soka Barani Afrika na waliopo sehemu mbalimbali nje ya Afrika walianza kuelekeza umakini wao nchini Cameroon hii ni kutokana na kuwepo kwa mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika
(AFRIKA) nchini humo mashindano ambayo kwa sasa yamefikia hatua ya robo fainali hii ni baada ya michezo ya hatua ya kumi na sita bora kutamatika usiku wa siku ya jumatano ya tarehe 26 mwezi huu wa kwanza.
Wakati mashindano hayo yanaanza mashabiki wa soka hapa nchini Tanzania walijikuta wanavutiwa sana kufuatilia mashindano hayo hii sio kwa sababu tu ya ukubwa wa mashindano yenyewe ambayo yanajumuisha wachezaji ambao wanacheza soka katika vikubwa zaidi duniani bali pia kwa kuwa wachezaji kadhaa kutoka katika vilabu vya soka hapa nchini Tanzania walikuwepo katika mashindano hayo wakiziwakilisha nchi zao.
Azam FC ndio timu iliyoongoza kwa kutoa wachezaji wengi kwa vilabu vya hapa nchini Tanzania hii ni baada ya wachezaji Bruce Kangwa, Prince Dube pamoja na Never Tigere kujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe ambacho kilishiriki mashindano hayo huku Simba ikitokea mchezaji mmoja ambae ni Peter Banda kwenda katika timu ya taifa ya Malawi na wakati huo Yanga ikitoa mchezaji mmoja pia yaani Djugui Diarra ambae aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Mali.
Huenda ni kwa sababu ya ukubwa na ushindani mkubwa uliopo katika mashindano hayo au ndio sehemu ya mchezo wa soka ambao una matokeo matatu kwa timu husika lakini katika hali ambayo mashabiki wengi wa soka hapa nchini Tanzania hawakuitarajia wachezaji wote kutoka ligi ya Tanzania bara wamejikuta wako nje ya mashindano hayo baada ya timu zao za taifa kufungwa na wapinzani wao.
Katika hatua ya makundi walianza wachezaji watatu wa Azam FC kutolewa yaani Dube, Kangwa na Tigere wakiwa na timu ya taifa ya Zimbabwe ambayo katika hatua ya makundi tu hali ikawa mbaya sana kwao na wakaaga mashindano hayo baada ya kushindwa kupata alama ambazo zingeifanya timu hiyo kutinga hatua ya kumi na sita bora ya mashindano hayo.
Peter Banda mchezaji wa timu ya soka ya Simba akiwa na timu ya taifa ya amejikuta akiaga mashindano hayo na timu yake ya Malawi baada ya kukubali kichapo cha magoli 2 kwa moja kutoka kwa timu ya taifa ya Morocco licha ya wachezaji wa timu ya Malawi kupambana sana lakini wakajikuta wanazidiwa maarifa na kufungwa katika hatua hiyo ya kumi na sita bora.
Djugui Diarra akiwa na timu ya taifa ya Mali na yeye usiku wa kuamkia Alhamisi akaungana na wachezaji wengine wanne kutoka katika timu za ligi kuu soka Tanzania bara kuaga mashindano hayo hii ni baada ya timu yake ya taifa ya Mali kufungwa na kutolewa na timu ya taifa ya Equatorial Guinea kwa mikwaju ya penati 5 kwa sita hii ni baada ya dakika 120 za mchezo huo kuisha bila ya kufungana.