QATAR 2022 NI CAMEROON, SENEGAL, GHANA, MOROCCO NA TUNISIA
MABALOZI wa Afrika kwenye Fainali za Kombe la Dunia baadaye mwaka huu nchini Qatar ni Cameroon, Ghana, Morocco, Senegal na Tunisia.
Cameroon imefuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya nane baada ya ushindi wa 2-1 ndani ya dakika 120 dhidi ya wenyeji, Algeria usiku wa kuamkia leo Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida.
Mshambuliaji wa Bayern Munich ya Ujerumani, Erick Choupo-Moting alianza kuifungia Cameroon dakika ya 22, hilo likiwa sawa na bao la kusawazisha baada ya Algeria kushinda 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Younde bao pekee la mshambuliaji wa Sporting Lisbon ya Ureno Islam Slimani dakika ya 40.
Mchezo ukahamia kwenye dakika 30 za nyongeza baada ya kutimua dakika 90 Cameroon ikiongoza 1-0 na mshambuliaji wa RKC Waalwijk ya Uholanzi, Ahmed Touba akaisawazishia Algeria dakika ya 118 likiwa sawa na bao la ushindi kwao kwa matokeo ya jumla.
Lakini wakati refa Bakary Papa Gassama wa Gambia anajiandaa kupuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo huku mashabiki wa nyumbani wakishangilia tiketi ya Qatar 2022, mshambuliaji wa Lyon ya Ufaransa, Karl Louis-Brillant Toko-Ekambi akazima kelele hizo kwa bao la dakika ya nne ya muda wa fidia baada ya kutimia dakika 120 za mchezo.
Ni Cameroon ya kocha Rigobert Song inakwenda Qatar baadaye mwaka ikiungana na Senegal, Ghana, Morocco na Tunisia kukamilisha idadi ya wawakilishi watano wa Afrika.
Mechi nyingine jana, Senegal walifuzu kwa ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Misri baada ya sare ya jumla ya 1-1.
Mechi ya kwanza Misri walishinda 1-0 Cairo, bao la kujifunga la Saliou Ciss dakika ya nne na jana Uwanja wa Me Abdoulaye Wade mjini Diamniadio, Senegal wakashinda 1-0 pia bao la kujifunga pia la Hamdi Fathi dakika ile ile ya nne.
Ni mshambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane aliyefunga penalti ya mwisho baada ya Ismaila Sarr na Cheikh Ahmadou Bamba Mbacke Dieng kufunga mbili zilizotangulia kufuatia Kalidou Koulibaly na Saliou Ciss kukosa mbili za mwanzo.
Kwa upande wa Misri, Mohamed Salah, Ahmed Mohamed Sayed 'Zizo' na Mostafa Mohamed wote walikosa huku Amr El Soleya pekee akiwafungia Mafarao.
Nayo Ghana imefuzu baada ya sare ya 1-1 na wenyeji, Nigeria jana Uwanja wa Taifa wa Abuja, hivyo kufuzu kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya 0-0 nyumbani kwenye mechi ya kwanza.
Ni Black Stars waliotangulia kwa bao la kiungo wa Arsenal, Thomas Partey dakika ya 10, kabla ya beki wa Watford ya England, William Paul Troost-Ekong kuisawazishia Super Eagles kwa penalti dakika ya 22.
Nayo Morocco ikaitandika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 4-1 na kufuzu kwa ushindi wa jumla wa 5-2 kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Kinshasa.
Mabao ya Morocco yalifungwa na Azzedine Ounahi mawili, dakika ya 21 na 54, Tarik Tissoudali dakika ya 45 na Achraf Hakimi dakika ya 69, wakati la DRC lilifungwa na Ben Malango Ngita dakika ya 77.
Tunisia ililazimishwa sare ya 0-0 na Mali Uwanja wa Olimpiki mjini Rades na kufuatia ushindi wa 1-0 ugenini kwenye mchezo ya kwanza nayo inakwenda Qatar.