Jeshi Laamuru Wachezaji Kurudisha Posho Baada ya Kushindwa AFCON.
Serikali ya taifa la Afrika la Magharibi la Guinea imewataka wachezaji wa timu ya taifa ya mchezo wa kandanda waliokuwa huko nchini Cameroon kurejesha pesa za marupurupu walizokuwa wamepewa endapo wangetwaa ubingwa wa AFCON 2021.
Hatua hiyo ya serikali ya Guinea inayo ongozwa na Kanali Mamady Doumbouya imekuja baada ya Wachezaji hao kutakiwa kulitwaa kombe la fainali za mataifa ya Afrika na mwishowe kushindwa kufanya hivyo.
Mambo yalivyokuwa kabla
Mwishoni mwa mwezi Disemba 2021, akiiaga timu ya taifa ya Guinea, Kiongozi mkuu wa taifa la Guinea,
Kanali Mamady Doumbouya aliwataka wachezaji wa timu ya taifa iliyokuwa ikienda kushindana katika fainali za AFCON 2021, kulitwaa taji hilo na wakishindwa, basi wazirejeshe pesa za posho walizokuwa wametengewa.
Kanali Mamady Doumbouya aliitetea kauli yake kwa kudai kuwa, serikali ya taifa hilo imewekeza pesa nyingi katika timu ya taifa, hivyo matokeo ya uwekezeji huo ni lazima yaonekane kwa kikosi hicho kulileta kombe la AFCON 2021 nchini Guinea.
Baada ya kufika nchini Cameroon
Mara baada ya kufika nchini Cameroon, timu ya taifa ya Guinea ilifanikiwa kupenya katika hatua ya 16 bora baada ya kushika nafasi ya pili katika jedwali la msimamo wa kundi B. Guinea ilipenya 16 bora pamoja na timu ya taifa ya Senegal huku Zimbabwe ikifungashwa virago na timu ya taifa ya Malawi kupita kama mshindwa bora.
Mchezo wa hatua ya 16 bora
Katika mchezo wa hatua ya 16 bora, Guinea ilipangwa kucheza na timu ya taifa ya Gambia. Kwa bahati mbaya, Guinea ilitolewa na Gambia kwa kufungwa bao moja kwa bila na timu ya taifa ya Gambia. Kushindwa kwa Guinea dhidi ya Gambia kulitamatisha agizo la Kanali Mamady Doumbouya kukitaka kikosi hicho kulipeleka kombe la AFCON 2021 nchini Guinea.
Wachezaji waparanganyika
Baada ya kutolewa na Gambia katika mchezo wa hatua ya 16 bora, Mara moja wachezaji wa timu ya taifa ya Guinea walisambaratika kwa kila mchezaji kurejea katika klabu yake bila ya kurejea nchini Guinea.
Kanali Mamady Doumbouya atangaza kuwasemehe
Baada ya kutolewa katika hatua hiyo ya 16 bora ya makala ya 33 ya fainali za mataifa ya Afrika huko nchini Cameroon, Kanali Mamady Doumbouya ametangaza kuwasemehe wachezaji wake wa timu ya taifa.
Pia, Kanali Mamady Doumbouya alieleza kuwa, kauli yake ya awali ya kukishurutisha kikosi hicho kulileta kombe la AFCON 2021 ililenga kukihamasisha kikosi cha timu ya taifa.
Azitaka pesa walizokuwa wamepewa za kufika hatua ya ¼ fainali, ½ fainali na fainali. Mbali na kutoa msamaha huo, Kanali Mamady Doumbouya amewataka viongozi wa timu ya taifa kuzirejesha hazina posho walizokuwa wamepewa endapo timu ya taifa ingetwaa taji hilo.
Kanali Mamady Doumbouya ameachana na pesa za kushiriki mchezo na zile za kufika hatua ya 16 bora na sasa anazitaka zile za ¼ fainali, ½ fainali na fainali (kutwaa taji) hatua ambazo timu ya taifa ya Guinea haikuweza kuzifikia.
Ikumbukwe kuwa, Kanali Mamady Doumbouya alitwaa madaraka mwezi Septemba 2021, baada ya kumpindua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Bwana Alpha Conde.
Kiasi cha pesa ambacho kinatakiwa kurejeshwa
Endapo wangefika hatua ya ¼ fainali, kila mchezaji wa timu ya taifa ya Guinea angelipwa shilingi milioni 23.
Wangefika hatua ya ½ fainali, kila mchezaji angelipwa shilingi milioni 28 na nusu.
Na wangefika hatua ya fainali na kutwaa taji, kila mchezaji angelipwa kitita cha shilingi za Kitanzania milioni 69.
Pesa zote hizo zikizidishwa kwa idadi ya wachezaji 30 wa kikosi hicho, kikosi cha timu ya taifa ya Guinea kinatakiwa kurejesha zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 3. 66 za posho na marupurupu.