Chama Aanza Vibaya Simba.
MARA baada ya kipyenga cha mwisho cha mchezo wa Ligi Kuu Bara kupulizwa, haraka mabosi wa Simba walifanya kikao cha dharura na benchi la ufundi la timu hiyo na wachezaji wote.
Hiyo ikiwa saa chache mara baada ya timu hiyo kutoka kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa ligi uliopigwa juzi Jumanne kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.
Kikao hicho kiliwashirikisha wachezaji wote akiwemo kiungo mpya wa timu hiyo, Mzambia Clatous Chama
aliyejiunga na timu hiyo wikiendi hii.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, viongozi wa timu hiyo waliitisha kikao hicho cha dharura kwa ajili ya kufanya tathimini ya mchezo wao dhidi ya Mbeya City.
Chanzo hichokilisema kuwa kikao hicho kilifanyika saa mbili usiku kabla ya chakula cha usiku huko Mbeya ambako mchezo huo ulipigwa. Kiliongeza kuwa mabosi wa timu hiyo waliwataka wachezaji hao kupambana katika michezo inayofuatia ili kuhakikisha wanapata ushindi utakaowawezesha kutetea taji lao la ubingwa wa ligi.
“Unaambiwa mara baada ya timu kupoteza mchezo wa ligi dhidi ya Mbeya City, uongozi wa timu hiyo uliokuwepo katika msafara, ulilazimika kukaa kikao cha dharura na wachezaji na benchi la ufundi.
“Kikubwa ni kuwaelekeza juu ya hatima ya matokeo hayo huku wakimtaka kocha kuhakikisha anasoma alama za nyakati kabla ya mchezo husika.
“Kikao hicho kilimtaka kocha huyo kujieleza na kutoa sababu ya kupoteza mchezo huo ambao ulikuwa ni muhimu kupata ushindi ili kuwaondoa kileleni wapinzani wao Yanga,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Barbara Gonzalez kuzungumzia hilo, kama kawaida yake simu yake ya mkononi iliita bila ya mafanikio kupokelewa.