Simba: Tunahujumiwa.
MMOJA wa mabosi wakubwa wa Simba ametamka kwa hasira jijini Dar es Salaam: “Tunahujumiwa.” Kisha akatangaza kufanya maamuzi magumu ndani ya siku tatu kuanzia Alhamisi.
Hiyo ni kufuatia matokeo mabovu ya Simba katika mechi tatu mfululizo zilizopita, yaliyowafanya wawe nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi 10 huku timu zote zikiwa zimecheza michezo sawa.
Kigogo huyo ambaye hakutaka kuanikwa na ambaye alisema habari hiyo ni siri, alilinyetisha Championi Ijumaa kuwa uongozi wa Simba umejipanga kufanya maamuzi magumu kabla ya Jumatatu juu ya mwenendo wa timu hiyo.
Simba imevuna pointi moja tu katika michezo yao mitatu iliyopita ambapo ilipoteza kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mbeya City kabla ya kutoka suluhu na Mtibwa Sugar, kisha ikapoteza kwa bao 1-0 juzi Jumatano dhidi ya Kagera Sugar.
Simba haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo zilizopita ambazo ni sawa na dakika 270 na kupelekea timu hiyo kubakia katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 25, nyuma ya wapinzani wao wa jadi Yanga wanaoongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi kumi wakiwa na pointi 35.
Bosi huyo ameeleza kuwa uongozi haufurahishwi na mwenendo wa timu na umedhamiria kufanya maamuzi magumu kabla ya siku ya Jumatatu kwa lengo la kurejesha makali yake kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara.
“Uongozi umesikitishwa na aina ya matokeo ambayo yamepatikana katika mechi tatu tulizocheza na ukweli ndani ya timu hali siyo nzuri kwa sababu siyo jambo la kawaida kupata pointi moja katika mechi tatu ambazo zilikuwa wazi kupata matokeo mazuri.
“Tunahisi kuna hujuma tunafanyiwa. Kilichopangwa na mikakati ilivyo kwa sasa ni kwamba uongozi utakutana ndani ya hizi siku tatu kuanzia leo (jana) Alhamisi, yaani haitafika Jumatatu watakuwa wamefanya maamuzi magumu ambayo hakuna anayejua kitu ambacho kinaweza kutokea,” alisema bosi huyo.
Bosi huyo hakuwa tayari kutaja kwa undani wanahisi wanahujumiwa kivipi, na kama hujuma hizo zinatoka ndani au nje ya Simba, kwa wachezaji au makocha, kwa viongozi au marefa.
Hata hivyo, alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Abdallah, alisema anaamini wamefanya vibaya kutokana na sababu za kiufundi, akisisitiza: “Hayo mambo mengine mi siyajui.”