Kilichotokea Baada ya Simba Kufungwa na Kagera.
Huenda walidhrika na mafanikio ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya kombe la Mapinduzi huko visiwani Zanzibar au ndio matokeo ya mchezo wa soka ambao kuna nyakati huwashangaza mashabiki wengi wa mchezo huo hii ni baada ya kupatikana kwa matokeo tofauti na watu walivyodhani hapo awali lakini ndio hivyo Simba baada ya kurejea kutoka visiwani Zanzibar wamejikuta wakifungwa katika mchezo dhidi ya
Mbeya City, kutoa sare na
Mtibwa Sugar na jumatano ya wiki hii wakafungwa tena na
Kagera Sugar.
Hukuwa na shabiki wa soka hususani shabiki wa
Simba ambaye angeamini kuwa timu hiyo itafungwa katika mchezo wao wa dhidi ya Kagera Sugar, hii ni kutokana na matokeo mabaya ambayo Simba wameyapata katika michezo miwili ya nyuma hivyo kuamini kuwa katika mchezo huo dhidi ya
Kagera, Simba ingepata ushindi ili kurejesha natumaini yao ya kuwania ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara ambao walitwaa msimu uliopita.
Dakika 90 za mchezo kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba mchezo ambao ulipigwa katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera uliisha kwa Simba kulala kwa goli 1 kwa bila hivyo kufanya Simba iwe imepoteza jumla ya alama 8 katika michezo 3 ya hivi karibuni na kuwapa nafasi Yanga ya kuwa juu ya Simba kwa utofauti wa alama 10 kwa sasa.
Baada ya Simba kusalimu amri na kuchapwa bao 1 kwa bila dhidi ya Kagera Sugar kuna mambo mbalimbali yamejitokeza katika ushindi huo wa Kagera Sugar dhidi ya Simba na kwa kuwa msomaji wangu napenda uwe karibu na masuala mbalimbali ya soka leo katika makala hii nimekusogezea mambo makubwa 4 ambayo yamejiri baada ya Simba kufungwa katika mchezo huo dhidi ya Kagera Sugar.
Jambo la kwanza, Simba hadi sasa imepoteza jumla ya michezo miwili ya ligi kuu huku magoli ya wapinzani katika michezo hiyo miwili yakiwa yamefungwa na wachezaji ambao wamewahi kucheza Yanga.
Simba kabla ya kuanza kufungwa katika michezo ya ligi kuu soka Tanzania bara ilifanikiwa kucheza jumla ya michezo 10 huku wakifanikiwa kushinda michezo saba na kutoa sare michezo 3 lakini katika mchezo wao wa 11 wakafungwa na Mbeya City huku goli la Mbeya City likifungwa na mshambuliaji Paul Nonga na katika mchezo wao wa kumi na tatu dhidi ya Kagera Sugar wakafungwa tena bao 1 huku bao la Kagera Sugar likifungwa na Hamisi Kiiza.
Miaka kadhaa iliyopita Paul Nonga aliwahi kucheza katika timu ya soka ya Yanga kwa msimu mmoja kabla ya kuondoka na hivyo pia kwa mfungaji wa goli la mchezo dhidi ya Kagera sugar yaani Kizza pia amewahi kucheza katika timu ya Yanga na kufanya makubwa kabla ya kuondoka nchini Uganda na kurejea nchini baada ya kusajiliwa na Simba.
Kizza na Paul Nonga wameweka historia ya kuwa wachezaji ambao waliwahi kucheza katika timu ya Yanga na kuifunga Simba katika michezo yote miwili ambayo Simba imepoteza hadi sasa.
Jambo la pili, kadi nyekundu ambayo Hamisi Kiiza ameonyeshwa katika mchezo dhidi ya Simba na kutolewa nje ndio kadi yake ya kwanza nyekundu katika historia yake katika mchezo wa soka.
Kizza Hamisi mchezaji wa Kimataifa wa Uganda katika nafasi ya ushambuliaji amekuwa akicheza soka kwa zaidi ya miaka kumi sasa katika vilabu mbalimbali ndani na nje ya Uganda huku kwa kipindi fulani alicheza Yanga na baadae Simba na sasa yuko katika klabu ya soka ya Kagera sugar ya mkoani Kagera.
Katika kipindi chote ambacho Kizza amecheza soka katika vilabu mbalimbali vya ligi kuu katika nchi mbalimbali Barani Afrika hakuwahi kutolewa nje kwa kadi nyekundu lakini katika mchezo huo, mwamuzi aliomuonyesha kadi nyekundu na kutoka nje katika dakika za nyongeza za mchezo huo na kuwa kadi yake ya kwanza nyekundu katika maisha yake ya soka.
Kizza alilisema hilo baada ya mchezo huo kuisha wakati akihojiwa na kuomba radhi mashabiki wa Kagera sugar kwa yeye kutolewa kwa kadi nyekundu licha ya kuipa goli la ushindi timu yake.
Jambo la tatu, kufungwa goli 1 na Kagera Sugar na kushindwa kupata hata bao 1 kwa timu ya Simba, kumemifanya Simba iwe imecheza jumla ya dakika 270 bila ya kupata goli katika michezo ya ligi kuu Tanzania bara.
Dakika 90 za mchezo kati ya Mbeya City dhidi ya Simba ziliisha kwa Simba kufungwa bao 1 kwa bila, dakika tisini zingine za mchezo kati ya Mtibwa sugar dhidi ya Simba ziliisha kwa sare ya bila kufungana na katika mchezo huo wa jumatano Kagera sugar walishinda goli 1 kwa bila huku Simba wakitoka bila goli.
Dakika 90 mara tatu ni sawa na jumla ya dakika 270 hivyo kuifanya Simba iwe imecheza jumla ya dakika 270 huku ikiwa na washambuliaji wake wote tegemeo bila ya kufunga hata goli 1 kitu ambacho ni adimu sana kukiona kwa Simba kwa miaka 5 ya hivi karibuni.
Ukiwa na washambuliaji kama Bocco, Mugalu na Kagere ambao msimu uliopita walifunga zaidi ya magoli 40 na sasa wamecheza kwa dakika 270 bila goli ni swala ambalo linatia mashaka sana na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo waanze kuwa na wasiwasi juu ya hali hiyo katika timu yao.
Jambo la nne, kadi nyekundu ambayo Kizza ameonyeshwa katika mchezo huo dhidi ya Simba umeifanya Simba iwe timu ya kwanza kucheza michezo mingi ya ligi kuu Tanzania bara huku wapinzani wao wakitolewa kwa kadi nyekundu.
Hadi sasa jumla ya wachezaji watano wa timu pinzani katika michezo ya ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Simba wametowa nje kwa kadi nyekundu hivyo kuifanya Simba iwe timu ya kwanza kucheza michezo mingi ya ligi huku wapinzani wao wakiwa pungufu kwa kutolewa wakati wa mchezo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu.
Mchezo dhidi ya Kagera sugar, mchezo dhidi ya Mbeya City, mchezo dhidi ya Coastal Union, mchezo dhidi ya Namungo FC na katika mchezo dhidi ya Dodoma jiji wachezaji wa timu pinzani walitolewa nje kwa kadi nyekundu na kumaliza mchezo wakiwa pungufu.
Huenda kwa sababu ya kucheza kwa kukamia sana au ufundi wa wachezaji wa Simba ndio inasababisha wachezaji wa timu pinzani kuonyeshwa kadi nyekundu lakini sio kadi nyekundu pekee hata adhabu ya penati msimu huu Simba ndio timu iliyopewa penati nyingi hadi sasa lakini wamekuwa na bahati mbaya ya kushindwa kufunga penati hizo.
Mashabiki, viongozi na wachezaji wa Simba kwa sasa hawapaswi kuanza kutengeneza migogoro kwa sababu ya matokeo mabaya ya timu hiyo badala yake kwa sasa wanapaswa kuendelea kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanatafuta njia ya kutatua changamoto ya matokeo mabaya ya timu hiyo na kurudi katika njia ya kusaka ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara.