Rafu hatari Ligi Kuu.
KUNA haja sheria 17 za soka kukumbushwa mara kwa mara kwa wachezaji ili kuepuka kufanyiana vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyoweza kuhatarisha maisha yao.
Madhara ya kucheza kwa utovu wa nidhamu yaliwahi kumuathiri aliyekuwa straika wa Yanga, Amissi Tambwe baada ya kukabwa na beki wa Ruvu Shooting, George Michael.
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilimfungia mechi tatu Michael kutokana na tukio hilo lililohatarisha maisha yake na tukio hilo lilikuwa Februari 2015.
‘Fair play’ ni moja ya kanuni za soka ambazo zinatakiwa kufuatwa ndani ya dakika 90 za mchezo kwa kila timu na mchezaji mmojamoja.
Licha ya sheria hiyo kuwepo, yapo baadhi ya matukio yanayojitokeza makusudi yakifanywa na wachezaji wenyewe kwa wenyewe yanayoonekana kuhatarisha maisha.
Kuna matukio manne ya ajabu msimu huu yamefanywa na wachezaji kwenye viwanja mbalimbali nchini. Mwanaspoti linakuletea baadhi ya matukio ya kushangaza yaliyofanywa na wachezaji na kuzigharimu timu zao.
SIMBA vs COASTAL UNION
Oktoba 31, 2021, katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Simba ilikuwa mwenyeji wa Coastal Union katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana.
Katika mchezo huo ilimlazimu mwamuzi Raphael Ikambi kutoka Morogoro kutoa kadi nyekundu kwa Henock Inonga wa Simba kwa kosa la kinidhamu alilomfanyia Issa Abushee.
Abushee alimvuta jezi Inonga akiwa katika harakati za kupambania mpira, kitendo kilichomfanya nyota huyo kumpiga kichwa na kutolewa kwa kadi nyekundu iliyoigharimu timu yake.
Mbali na Inonga katika mchezo huo Jacob Junior alilimwa kadi nyekundu kutokana na faulo kwa kosa la kujitakia akipiga mpira kwa hasira kabla ya mwamuzi kuamuru ikawa kadi ya pili ya njano baada ya awali kuonywa kwa kushindwa kucheza mchezo wa kiungwana kwa Sadio Kanoute.
POLISI TANZANIA vs YANGA
Mchezo uliokuwa na upinzani mkali kwa timu zote mbili ulipigwa Januari 23 Uwanja wa Sheikh Amir Abeid, Arusha huku Yanga ikish-inda bao 1-0.
Katika mchezo huo beki wa Yanga, Djuma Shaaban
alimchezea rafu ya makusudi nyota wa Polisi Tanzania, Yahya Mbegu akimpiga kiwiko usoni na kugalagala chini.
Licha ya uwepo wa waamuzi wanne ndani ya mchezo, lakini hawakuliona tukio hilo hadi baada ya video ya mchezo huo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha tukio hilo. Djuma amefungiwa mechi tatu na faini ya Sh1 milioni.
SIMBA vs NAMUNGO
Novemba 3, mwaka jana, Simba ilicheza na Namungo katika Uwanja wa Mkapa ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika mchezo huo mwamuzi Nassoro Mwichui alitoa kadi nyekundu kwa beki wa Namungo, Abdlulaziz Makame aliyemchezea rafu Shomary Kapombe ambayo huenda ingemsababishia madhara makubwa kwenye mguu wake.
Ilikuwa dakika ya 50 ya mchezo huo ambapo Makame aliigharimu timu yake ikicheza pungufu ingawa baadaye aliomba msamaha kwa Kapombe.
BIASHARA UNITED vs SIMBA
Mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ambao Simba ilitoka sare ya bila kufungana, beki wake Kennedy Juma alionyesha mchezo usiokuwa wa kiungwana kwa Christian Zigah.
Baada ya tukio hilo ilimlazimu mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kumpa kadi ya njano kwa kumpiga mwenzake teke la mgongoni.
Tukio hilo lilitokea dakika za nyongeza za mchezo huo baada ya John Bocco kukosa mkwaju wa penalti iliyosababishwa na Pape Sakho aliyechezewa rafu na Salum Kipaga.
Staa wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala anasema wachezaji wanapokuwa uwanjani damu zao zinakuwa zinachemka, hivyo anaweza akafanya lolote na kinachokuwa kinatakiwa kufanywa ni wenzake kumtuliza.
“Mchezaji akiwa amechemka na akafanyiwa kitu kitakachomkasilisha anakuwa nusu mtu na nusu jini. Anaweza akafanya lolote baadaye akitulia anajuta. Kikubwa ni wachezaji waepuke vitendo vya utovu wa nidhamu,” anasema.
Samuel Mpenzu, mwamuzi wa zamani wa soka anasema muda mwingine unakuta mchezaji hajaonwa na mwamuzi, lakini ikaonekana kwenye runinga na wachezaji huwa wajanja kuvizia mwamuzi jicho lake liko upande gani ili kufanya tukio wanalokusudia.
“Wachezaji wajanja sana kusema kweli. Unakuta mwamuzi muda mwingine hajaona tukio...wajitahidi kujirekebisha hizi tabia sio nzuri hata kidogo, maana mchezaji anaweza kuhatarisha maisha ya mwenzake,” anasema.