Kaseja: Silogi mtu ni uwezo tu.
MIAKA 20 kwenye Ligi Kuu Bara, Juma Kaseja anajua siri nyingi za soka la Bongo na utamdanganya nini kuhusu mpira wa nchi hii? Huyu ni gwiji.
Tanzania One, Mikono Mia, mfano wa kuigwa, kipenzi cha wengi ni kati ya sifa nyingi ambazo amekuwa akipambwa nazo supastaa huyu wa soka nchini. Kiufupi, Juma K. Juma si mtu wa mchezo mchezo
Amekipiga kwa kiwango cha juu katika klabu kubwa nchini za Simba na Yanga, pia akizitumikia Moro United, Mbeya City, Kagera Sugar na sasa KMC huku pia akijenga heshima kubwa kwenye timu ya taifa, Taifa Stars, ambako alifahamika kwa jina la Tanzania One.
Ukibahatika kukaa na supastaa huyu, utagundua ni mcha Mungu, mcheshi, mkarimu, anajali utu kuliko vitu, nidhamu na bidii ni silaha ya mafanikio yake.
Mwanaspoti ilifunga safari kutoka Tabata Relini hadi Bunju kwenye kambi ya KMC ambako timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni imejichimbia na kubahatika kuongea na staa huyo ili kufahamu mengi ndani ya maisha yake ya soka.
Ukisikia maneno ya watu nje na kumtazama mwonekano wake, unaweza kudhani ni mtu wa majivuno lakini kumbe sivyo hata kidogo na ndio maana wahenga walisema usihukumu kitabu kwa kuangalia kava, kisome ndani.
Kama haujui ndivyo ninavyokujuza Kaseja, ni moja ya wachezaji wanaojua nini wanatakiwa kukifanya na kwa wakati gani ili kuepuka kukwazana na nyota wenzake pamoja na viongozi.
Kaseja anasema, jina kubwa alilonalo mpaka sasa, sio fimbo ya kujivunia kuwachapia wenzake bali anaamini alipo hivi sasa ni mapenzi ya Mungu.
“Mimi kwanza sipendi kumdharau na kumchukia mtu japokuwa mimi wananidharau na kunichukia lakini wanaofanya hivi ni kwa sababu hawanijui mimi Juma nikoje na wengine wananunua chuki bila sababu,” anasema.
SILOGI UWEZO TU
Mkongwe huyo aliyecheza kwa mafanikio makubwa na ameweka wazi changamoto alizokutana nazo huku imani za kishirikina akitaja kuwa ndio ishu iliyomsumbua zaidi na kusema lakini haikumuumiza sana kwani hakuwahi kufanya vitu alivyokuwa anahusishwa navyo.
Anasema alikuwa akihusishwa mara kwa mara kwenye imani hizo huku akitaja Mungu kuwa ndio alikuwa kimbilio lake kwenye kazi yake hiyo japo lawama zilikuwa nyingi kwake hakuzipa nafasi majibu yake yalikuwa kwa maandishi na sio mdomo.
“Unaweza kufanya kitu na watu wasione, na mimi nilikuwa naandika ujumbe kwenye fulana yake kwamba Kaseja atabaki kuwa Kaseja kwa hiyo zile jumbe zilikuwa za watu ili kuheshimu wenzao kutokana na juhudi wanazoonyesha kwa kuachana na kashfa ambazo hazikuwa na maana,” anasisitiza.
Kaseja anasema alikuwa anavaa nguo nyeupe zenye ujumbe ndani ya jezi akifanya vizuri mpira unapoisha anavua jezi anabaki na ujumbe wake uliokuwa ukisomeka kuwa yeye atabaki kuwa yeye miaka yote kutokana na juhudi zake na sio imani za kishirikina wanazomtwisha.
“Mpira wetu wa Tanzania una changamoto nyingi kwa upande wangu nimeweza kupambana nazo na kufanikiwa kufika hapa nilipo kama ningekuwa mtu wa kuka tamaa nadhani ningekuwa nimeshastaafu soka, halafu ishu ya ushirikina ingekuwa na maana basi mimi ningedaka hadi Barcelona,” anasema.
DALADALA FRESH TU
Kwa upande wa wachezaji wa Tanzania wakitaka kuonyesha kama wamefanikiwa basi ni kumiliki dinga, lakini unaambiwa kwa upande wa Kaseja yeye anaona kujionyesha ni ulimbukeni akisisitiza yeye ni sawa na binadamu wengine hivyo hana sababu za kujitofautisha na ndio maana usafiri wake mkubwa ni daladala.
“Nimeanza kumiliki gari 2002 lakini sioni maajabu japo nimekuwa nikichukuliwa tofauti na wachezaji wengi kwa kuniona natumia usafiri wa umma. Kwani mimi nina utofauti gani na wengine hadi nijiweke mtu wa juu zaidi yao,” anasema, Kaseja ambaye anamiliki nyumba kadhaa na magari kadhaa amba-yo mwenyewe hataki kuyazungumzia akisema hayo ni maisha yake binafsi sana.
Anakiri kuchukizwa na watu wanamuita na kumuona staa wakati yeye hana ustaa wowote na ni binadamu wa kawaida kama ambavyo binadamu wengine wanaishi.
“Mimi sipendi kabisa, sijui ustaa ndio nini na unanisaidia nini naishi maisha ya kawaida kama ambavyo wengine wavyoishi sio kwamba gari sina hapana, sina tabia za kupanda bodaboda wala mwendokasi hapana naamua tu na napenda sana kusema ukweli,” anasema Kaseja.
Kaseja anasema, licha ya watu kumshangaa na wengine kumuona amefulia yeye anaona ni sawa tu kwa kuwa maisha yake anayeyajua ni Mungu pekee lakini mwanadamu ni ngumu.
LAKI 2 MORO UTD
Anasema ulikuwa usajili wake wa kwanza katika maisha yake ya mpira, ambapo aliipokea pesa hiyo akiwa na majonzi kutokana na msiba wa baba yake mzazi.
Anasema wakati wanaondoka kumbe nyuma jamaa wa Moro United walipishana wakawafuata mpaka Magomeni, kwenye moja ya baa maeneo hayo wakati huo inaitwa Zaragoza ambayo sasa Moro United.
“Nilisaini laki 2 mwaka 2000 Novemba ikiwa daraja la kwanza, nakumbuka kaka alivyowaambia nimefiwa wakaniongezea Sh50,000 nakumbuka hiyo pesa yote nilimpa mama yangu baada ya kwenda msibani kumzika baba,” anasema Kaseja.