Mabosi Simba waapa sasa ni mwendo wa kugawa dozi.
SIMBA haina matokeo mazuri katika mechi zake tatu za Ligi Kuu Bara ingawa wikiendi iliyopita walirejesha ubabe wao nyumbani wakiipasua Dar City na kudhihirisha bado jamaa wana utamu wao.
Kama umeshtuka, Simba imeyumba mechi tatu za ligi ugenini ambako ndani ya dakika 270 hizo wamevuna pointi moja pekee iliyotokana na sare dhidi ya Mtibwa Sugar huku wakipoteza dhidi ya Mbeya City kisha Kagera Sugar.
Hata hivyo, mechi hizo sasa zitasimama kwa muda na Simba itarejea uwanja wake wa heshima wa Mkapa na katika ligi mechi yao ya mwisho kucheza hapo ni walipoichapa Azam FC siku ya kwanza ya mwaka 2022 mabao 2-1. Na wakati ikijiandaa kurudi kwa Mkapa, mashabiki wanatamba wakiwaambia wapinzani wao wajao kwamba wataona, hatoki mtu.
Walianza kwa kutuma salamu kwa kuangusha kipigo kizito kwa Dar City cha mabao 6-0 kwenye Kombe la Shirikisho la Azam.
Simba sasa itaendelea kudumu nyumbani hapo kwa Mkapa na watu wakae sawa kwani jamaa wana dakika 450 za kurudisha ubora baada ya ratiba yao kufumuliwa kidogo.
Simba watawakaribisha wachovu Tanzania Prisons kesho Alhamisi mchezo ambao awali ulipangwa upigwe Februari 6 na hapo kutakuwa na vita ya wekundu hao kutakiwa kuendelea kufuta machozi ya wanachama na mashabiki wao walioumizwa na sare na vipigo viwili.
Wakimaliza hapo watarudi katika maandalizi yao kisha kurejea uwanja huohuo dhidi ya Mbeya Kwanza Februari 6 na badaa ya hapo watahamia Kimataifa wakiwakaribisha Asec Mimosas ya Ivory Coast katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya hapo Simba itasafiri kwenda ugenini wakiwafuata Union Sportive Gendarmerie Nationale (USGN) ya Niger katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi kisha kurejea tena nyumbani kuikaribisha Biashara United mchezo wa Ligi Kuu
Kwa upande wa viongozi wa klabu hiyo, umesema sasa wamejipanga kupata pointi tatu kila mchezo uliombele yao.
“Tumebakiza michezo miwili kabla ya kumaliza mechi za mzunguko wa kwanza. Tumejipanga kupata pointi zote sita kwenye mechi hizo na kuanza mzunguko wa pili kwa nguvu mpya,” alisema Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu.
Alisema wamepata matokeo ya kuumiza katika mechi zao tatu mfululizo, lakini haiwezi kuwarudisha nyuma, Simba itaendelea kupambana kuhakikisha inafanya vyema mechi zijazo.