Pablo atikisa Simba, ataka majembe matatu
KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco hataki utani, anataka timu hiyo ibebe ndoo ya tano mfululizo na ameainisha mengi kwenye ripoti yake ikiwamo kuimarisha benchi lake la ufundi na kuleta wachezaji mashine wapya watatu.
Pablo ameuomba uongozi wa klabu hiyo kumpa nafasi ya kuwaleta wasaidizi wake katika benchi la ufundi, hatua ambayo inaweza kufagia benchi lote la kina Selemani Matola na Thierry Hitimana, kama alivyotaka wakati akipewa dili hilo la kufundisha Msimbazi kwa mara ya kwanza.
Awali, uongozi wa Simba ulimuomba umpe muda wa kuwaangalia waliopo kwa miezi mitatu kabla ya kuongeza watu wapya.
Ni miezi miwili tu sasa tangu amefanya kazi na wasaidizi wake Hitimana na Matola, lakini Pablo anaona bado Simba inaweza kuboresha zaidi benchi hilo na kuifanya Simba iwe timu ya kutisha zaidi.
Pablo anataka kufanya kazi na benchi lake jipya na ikishindikana abaki japo na mmoja kati ya Matola au Hitimana,
Chanzo cha kuaminika ndani ya Simba kimelithibitishia gazeti hili kuwa Pablo anataka benchi lake liimarishwe.
“Kocha amesema anapenda kocha ambaye atamsaidia kwa vitendo na sio maneno, tangu ametua Simba amekuwa akisaidiwa kwa ukaribu zaidi na kocha wa viungo Daniel De Castro ambaye ni pendekezo lake mwenyewe ndani ya timu hiyo,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake liandikwe gazetini.
“Kocha anapenda kuchagua kikosi kwa njia ya michoro, anaamini makocha watakaokuja kuongeza nguvu watamsaidia sana katika hilo,” alisema.
Alisema katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili uongozi ukitumie pia kumtafutia wachezaji watakaoboresha timu.
MAJEMBE MATATU
Katika kuhakikisha malengo ya kutisha kwenye Kombe la Shirikisho na kubeba taji la tano mfululizo la Ligi Kuu Bara yanafanikiwa, mabosi wa Simba wapo katika mawindo makali kwenye nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika kwa ajili ya kufanyia kazi ripoti ya kocha wao mkuu, Pablo Franco aliyeeleza anataka majembe matatu mapya.
Mwanaspoti limejiridhisha katika majembe hayo matatu tayari mmoja ameshapatikana ni kiungo fundi kutoka RS Berkane ya Morocco, Mzambia Clatous Chama ambaye muda wowote atakuwa hapa nchini kujiunga na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Wakati mabosi hao wa Simba wakiendelea kusaka mashine hizo nyingine mbili mpya, huenda wakafanya uamuzi mgumu wa kuachana na beki wake mkongwe, Erasto Nyoni ambaye hakuwepo katika orodha ya hapo awali.
Inaelezwa mabosi hao wa Simba wametoa ruhusa kwa timu ambayo itamtaka Nyoni Erasto kutuma maombi rasmi ya barua na wapo tayari kumuachia hata kwa mkopo kama ilivyo kwa nyota wengine wanne.
Nyota hao wengine wanne ambao huenda nao wakawa wamekalia kuti kavu na wakatolewa kwa mkopo ni Pape Ousmanne Sakho, Pascal Wawa,Abdulsamad Kassim na Duncan Nyoni.
Alipotafutwa Abdulsamad alisema alikuwa sehemu ya kikosi kilichokwenda Bukoba kwa ajili ya mchezo wa Kagera Sugar: “Bado sijapewa taarifa ya kwenda kwa mkopo katika timu nyingine.”