Huyu Chico ni Balaa.
CHICO Ushindi, ingizo jipya ndani ya Yanga, ameanza kwa ushindi kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Mbuni FC mbele ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.
Juzi, Chico alicheza kwa mara ya kwanza mchezo wa kirafiki na ubao wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ulisoma Mbuni 0-2 Yanga na mabao yote yalifungwa kwa penalti na mtupiaji alikuwa ni Tonombe Mukoko.
Chico alianzia benchi na aliingia dakika ya 64 akichukua nafasi ya Deus Kaseke na katika dakika 64 aliweza kufanya makeke yake yaliyoonyesha kwamba ikiwa ataendelea na kasi hiyo, atakuja kuwa ni chaguo la kwanza. Alisababisha penalti moja dakika ya 81 baada ya kuchezewa faulo na nyota wa Mbuni ndani ya 18 na iliweza kufungwa na Mukoko, ilikuwa dakika ya 82.
Pia alikuwa na uwezo wa kupiga pasi zenye uhakika kwa kuwa pasi zake zote alizopiga ziliwafikia wachezaji kwa asilimia 100 na aliweza kupiga jumla ya pasi 13.
Hakuwa mnyonge kwenye eneo la kumiliki mpira na kutembea nao kwa kuwa aliweza kufanya ‘dribble’ 7 huku mguu anaopenda kuutumia ni ule wa kulia na ameonekana kuwa siyo winga mchoyo kwa kuwa hata akiwa ndani ya 18, anatoa pasi.
Mkongomani huyo alitambulishwa rasmi na Yanga Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, ambapo Yanga walikuwa na mchezo wa ligi ugenini dhidi ya Coastal Union uliomalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema: “Matokeo ya ushindi kwenye mchezo wetu dhidi ya Mbuni yamekuwa muhimu kwa ajili ya kuwaandaa wachezaji wetu kisaikolojia, hasa wale ambao wamekuwa hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kuelekea michezo yetu ijayo ya Ligi Kuu Bara.
“Kuhusiana na uwezo wa Chiko Ushindi, alichokionyesha Jumatano ni sehemu ndogo tu ya ubora wake, ameanza vizuri na kuonyesha maelewano mazuri na wenzake na hii inaonyesha ni wazi kuwa atawahi kuingia kwenye mfumo na kutoa changamoto kwa Saido Ntibazonkiza na Jesus Moloko kwenye kikosi cha kwanza.”
Naye kiungo wa zamani wa Simba, Amri Kiemba amefungukia kiwango cha nyota huyo huku akikiri kuwa anajua.
Kiemba alisema kwa dakika chache ambazo amemshuhudia winga huyo akicheza, amebaini kuwa ni mchezaji mzuri ambaye ataongeza kitu ndani ya klabu hiyo. “Ushindi ni mchezaji mzuri, kwa dakika chache nilizomuona nimegundua kuwa ana uwezo mzuri wa kupiga krosi zenye macho, lakini pia ana uwezo mzuri wa kupiga pasi zenye macho.
“Mbali na hapo ni mchezaji mwenye uwezo wa kukokota vizuri mpira, hivyo naamini ataongeza kitu ndani ya Yanga, japo bado unahitajika muda mwingi zaidi kuthibitisha kama yeye ni bora,” alisema kiungo huyo.