Yanga yeyote anakupiga, Nabi akusanya washambuliaji 15.
JESHI la Yanga lipo kambini Avic, Kigamboni likijiwinda na mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Biashara United, kabla ya kuliamsha tena katika Ligi Kuu, huku ikibainika namna Kocha Nasreddine Nabi alivyo mjanja.
Yanga Jumanne itarudi uwanjani kuvaana na Biashara katika mechi ya 16 Bora, jijini Dar es Salaam, ikiwa kwenye mawindo yao ya kutaka kubeba mataji ya michuano pekee iliyonayo mkononi kwa sasa, Ligi Kuu iliyolikosa kwa misimu minne mfululizo na lile la ASFC misimu mitano mfululizo. Yanga ilibeba ASFC msimu wa 2015-2016 wakati katika ligi ni 2016-2017.
Katika kuhakikisha wanafanikisha jambo lao kwa msimu huu, mabosi wa Yanga chini ya maelekezo ya kocha wao, Nabi imesajili jumla ya washambuliaji 15 na hadi sasa wameshatupia mabao 23 katika ligi na mengine matano ya ASFC.
Washambuliaji hao wanaojumuisha viungo washambuliaji, mawinga na mastraika ni pamoja na wale wapya wakiongozwa na Heritier Makambo, Fiston Mayele, Jesus Moloko, Chico Ushindi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Khalid Aucho, Yusuf Athuman, Denis Nkane na Crispin Ngushi.
Awali kulikuwa na Deus Kaseke, Dickson Ambundo, Saido Ntibazonkiza, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Yacouba Songne na Mapinduzi Balama aliyekuwa majeruhi wa muda mrefu kabla ya kurejea uwanjani hivi karibuni.
Uwepo wa washambuliaji wengi umefanya kila eneo kuwa na wachezaji watatu wa maana hali iliyomrahisishia Nabi hata pale mchezaji mmoja anapokosekana kwani mbadala wake anakuwepo.
Mayele ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi akiwa nayo sita, kati ya 23 ya timu yake katika ligi, huku akiwa na jingine moja kwenye ASFC, akifuatiwa na Saido Ntibazonkiza na Fei Toto wenye manne kila mmoja, Moloko, Aucho wenye matatu kila mmoja, huku Dickson Ambundo akiwa na moja sawa na beki Djuma Shaban na kiungo mkabaji aliyetimka TP Mazembe ya DR Congo, Mukoko Tonombe.
Nkane aliyesajiliwa kutoka Biashara, hajafunga lakini alitua akiwa na mabao mawili katika ligi, huku Ngushi naye akiwa na matatu aliyotoka nayo Mbeya Kwanza kuonyesha nao gari likiwaka Yanga itakuwa moto mkali zaidi.
TIZI KALI
Huko kambini Avic, Yanga imeendelea kujifua na mastaa wake wakionyesha kuwa na mzuka mwingi kwa mechi zijazo.
Mechi dhidi ya Biashara ni ya tatu kwa timu hizo kukutana katika ASFC itapigwa kuanzia saa 1 usiku, ili kuamua timu ipi ya kwenda robo fainali. Katika mechi za awali Yanga iliishinda Biashara katika 16 Bora ya 2019-2020 kwa penalti baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 2-2 kisha msimu uliopita kuing’oa nusu fainali kwa 1-0.
Kocha Nabi ameonekana kuvutiwa na nyota wake wanavyojituma mazoezini na kutimiza kile anachowaelekeza na wasaidizi wake.
WADAU WAFUNGUKA
Mshambuliaji wa zamani Yanga, Herry Morris alisema kikosi hicho kwa misimu mitatu kilikuwa hakina washambuliaji wazuri, walipokuwepo wakipata majeraha ilikuwa changamoto tofauti na sasa.
Morris alisema nyuma eneo la ulinzi lilikuwa hakuna tabu sana kama ilivyokuwa eneo la ushambuliaji, hali hiyo imewafanya viongozi wajitathimini na kugundua makosa yaliyopo.
“Licha ya kwamba wanafanya vizuri bado wanatakiwa kuongeza mkazo kwenye kumalizia nafasi eneo hilo kwa sababu wanatengeneza nafasi nyingi na wanazitumia chache, eneo hilo washambuliaji waongeze umakini.”
Naye mshambuliaji wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella alisema “Misimu miwili mitatu nyuma hawakuwa na washambuliaji wengi na sasa
wameona wafanye usajili eneo hilo kwa nguvu kubwa na imeonyesha kabisa wamefanikiwa kwa kiasi fulani,” alisema Mogella, huku Bakar Malima ‘Jembe Ulaya’ akisema; “Misimu miwili au mitatu nyuma iliyoisha hawakuwa vizuri kwenye maeneo hayo na ndio maana msimu huu wamefanya usajili eneo la kati (kiungo), ushambuliaji na umeonyesha kuna faida.”