Mbinu zilizoibeba Simba kuiua Asec.
HII ndio Simba. Achana na kikosi cha Simba ambacho kinapata ushindi wa kusuasua Ligi Kuu Bara, lakini kwenye mashindano ya kimataifa wameanza na moto.
Simba ndio wawakilishi pekee wa Tanzania kimataifa na juzi walianza vizuri Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Asec Mimosas.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wapo katika hatua ya makundi na ushindi huo una maana kubwa kwao kwani michezo miwili inayofuata wanacheza ugenini dhidi ya USGN na RS Berkane.
Katika mechi ya juzi, Simba kipindi cha kwanza walitangulia kwa bao 1-0 hadi mapumziko lililofungwa na Pape Ousmane Sakho, lakini haya ndio yaliyoibeba Simba katika mchezo huo.
ASEC 10 NYUMA
Katika mchezo huo, Asec waliingia na plani ya muda mwingi kujilinda na walikuwa na wachezaji tisa mpaka kumi katika eneo lao la kujilinda ili kuwapa Simba wakati mgumu kufunga bao.
Baada ya Simba kufunga bao lilitokana na krosi ya Shomary Kapombe na Sakho kufunga kwa mtindo wa aina yake wa tiki taka ndipo Asec walianza kufunguka na kwenda kushambulia na kuacha kucheza kwa kujilinda zaidi.
Ukiachana na Asec, timu zingine ambazo Simba imecheza nazo msimu huu katika Ligi Kuu Bara zikicheza kwa mfumo huo ni Coastal Union, Mbeya City, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar.
KIUNGO NOMA
Kipindi cha kwanza eneo ambalo Simba walifanikiwa kutawala na kuzalisha bao lilikuwa la kiungo ambalo walianza Jonas Mkude, Sadio Kanoute na Rally Bwalya .
Pale walipocheza eneo hilo Simba walianzisha mashambulizi hatari ikiwemo shuti la chini lililopigwa na Meddie Kagere likagonga mwamba wa goli la Asec.
Kutawala kwa Simba eneo la katikati kulianzisha shambulizi lingine hatari ambalo lilitumiwa na Sakho kufunga bao akiunganisha krosi ya Kapombe.
Simba walipojaribu kushambulia kwa mipira mirefu bila kupitia katika eneo la kati hawakuwa na madhara zaidi na walipoteza mipira mara nyingi.
Ubora wa Sakho aliyecheza kwa dakika 40 na kutolewa akingia Mzamiru Yassin ulikuwa katika kiwango bora na aliwasumbua mabeki wa Asec kila alipokuwa na mpira.
NAFASI MURUA
Simba katika mechi hiyo miongoni mwa mambo ambayo walifanikiwa kutawala ni kucheza katika maeneo tofauti na kuyamiliki kwa kupiga pasi ndefu na fupi za uhakika.
Kucheza huko kwa Simba kuliwapa nafasi ya kufunga mabao matatu, lakini muda waliolazimisha kucheza kwa aina tofauti kama ile mipira ya juu hawakufanikiwa walipoteza mipira mingi.
Kucheza huko kwa Simba kuliendelea kuimarisha ubora wa kikosi hicho kwani walitengeneza nafasi sio chini ya tatu kwa wachezaji tofauti, ila walipoteza kutokana na kukosa utulivu na umakini.
Miongoni mwa nafasi ambazo Simba walikosa kuzigeuza kuwa mabao ni ile ya Meddie Kagere, Peter Banda, Rally Bwalya na nyinginezo.
KUJIAMINI ZAIDI
Miongoni mwa makosa ambayo yanaendelea kuwagharimu Simba msimu huu ni mabeki kucheza kwa kujiamini mara baada ya kuwa mbele kwa matokeo.
Kujiamini huko kulimfanya beki Joash Onyango kufanya kosa ambalo halikuwa na ulazima kupoteza mpira mbele ya mchezaji wa Asec, Aziz Stephane na kupata urahisi kufunga bao la
kusawazisha. Kosa hilo la kucheza kwa kujiamini zaidi kwa mabeki sio tu kwa Onyango, bali hata Henoc Inonga amekuwa akifanya hivyo kwenye baadhi ya mechi za mashindano.
Onyango na Inonga wanatakiwa kubadilika haraka katika aina hiyo ya uchezaji kwani wasipobadilika wanaweza kujikuta wanaigharimu zaidi timu yao.
MABADILIKO SIMBA
Baada ya Asec kupata bao la kusawazisha walikuwa wakicheza kwa kujiamini na kuendelea kuimarisha eneo la ulinzi ambalo halikuwa linafanya makosa mara kwa mara.
Benchi la ufundi lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mabadiliko ya ya pili kuingia John Bocco na Yusuph Mhilu.
Bocco aliyekuwa katika kiwango bora kwa dakika alizochezea alihusika na mabao mawili yaliyowapa Simba ushindi wa kwanza wa michuano hiyo. Bao la pili ambalo lilikuwa la penalti lilitokana na uhodari na kujitoa kwake alipokwenda kuchukua mpira kwenye mstari wa kutoka na kupiga krosi ambayo kipa wa Asec alishindwa kuokoa vizuri mpaka kumchezea rafu Mhilu ndani ya boksi na mwamuzi kuamuru kuwa ni penati uliyopigwa na Kapombe.
Ubora wa kuomba mpira kwenye njia, uharaka na utulivu mkubwa aliokuwa nao Bocco ulizaa bao la tatu lililotokana na krosi ya maana aliyopigia Banda aliyefunga bao la tatu.
MAKOCHA HAWA HAPA
Akizungumzia mchezo huyo, Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema ilikuwa mechi ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wao ambao waliingia na mbinu za kuwazuia na kuhakikisha hawafanyi vizuri.
“Wapinzani walikuwa katika kiwango bora. Tulibadilika aina yetu ya uchezaji ili kupata pointi tatu dhidi yao na tulifanikiwa hilo,” alisema Pablo.
“Mechi hii imetupa mwanga kuelekea nyingine zilizo mbele kwani tunaenda kucheza ugenini na huko tunatafuta pointi kama ilivyokuwa nyumbani.”
Kocha wa Asec, Julien Patrick alisema ilikuwa mechi ngumu na walifanya makosa yaliyowarahisishia Simba kufunga mabao mawili ya haraka yaliyoamua mechi.
“Kuna wakati katika kipindi cha pili tulishika mchezo, tulikuwa na uwezo wa kushinda ila ubora wa Simba hasa katika eneo la kiungo ulichangia ku tuzidi,” anasema Patrick.