Mwameja afichua siri nzito Simba
KATIKA sehemu zilizotangalia, kipa gwiji wa soka wa Simba na Taifa Stars, Mohammed Mwameja alizungumzia usajili wake Yanga ulivyokaribia kumtoa roho kabla ya dili hivyo kufa, ugomvi wake na Ndolanga ambao hawakusuluhishwa hadi kigogo huyo akafariki dunia na ile stori ya kuuza matikiti Uingereza badala ya soka. Endelea…
MWAMEJA ambaye sasa ni mjasiriamali akisisitiza kuwa anapenda kujiita Mmachinga anayefanya biashara zake Temeke, Dar es Salaam amesisitiza kuwa hobi yake ni soka na aliondoka Simba akiwa bado anapenda mpira na akiwa kwenye kiwango bora.
“Yaliibuka maneno maneno baada ya mechi yetu moja tuliyotwaa ubingwa, ile mechi tuliicheza katika mazingira magumu, wachezaji ndiyo tulibeba jukumu la kusafirisha timu, viongozi walikuja kwenye fainali.
“Tuliposhinda, pesa wakapewa viongozi, wakati wa kugawa wakataka baadhi ya wachezaji wapewe 300,000 na wengine 150,000, nilikataa nikasema kitu hicho hakipo, wote tupewe Sh300,000 hapo nikaonekana mjeuri na hiyo ndiyo ilikuwa moja ya vitu vilivyosababisha niondoke Simba na kuamua kustaafu,” anasema.
MSOTO WA SIMBA
Mwameja anasema ukiwa nahodha wa Simba wakati ule ilikuwa ni kama kiongozi, kuna muda unabeba jukumu la kutafuta fedha ili mambo ya timu yaende.
“Tumepitia maisha magumu, wakati ule klabu imecheza sana ndondo ili kupata huduma muhimu, kuna muda mko njiani basi la timu halina mafuta, hamjui mtakula nini, hivyo unalazimika kama nahodha kuomba msaada kwa wapenzi au timu icheze ndondo ili mambo yaende,” anasema.
“Wakati ule hakukuwa na mshahara, baadaye mwaka 1993 ndiyo tulikuja kupewa tena sio wachezaji wote, nakumbuka mshahara wangu wa kwanza ilikuwa Sh100,000 kisha 120,000 na ni mtu tu aliamua kutoa kama yeye na sio klabu.
“Kabla tulikuwa tunapata bonasi kwa kila mechi, kulikuwa na mkataba wachezaji na uongozi, kabla ligi kuanza mnazungumza kwa maana kwamba ili tuchukue ubingwa, lazima mshinde hivyo tunaposhinda mechi moja bonasi ni asilimia 60, tukitoka sare ni asilimia 30 na tukifungwa ni asilimia 10, hivyo mishahara yetu tulikuwa tunaitengeneza kwa hivyo.
“Wachezaji tuliishi kwa staili ya kutengeza hamasa ili mashabiki wajae uwanjani, kuna muda unaweza kusikia baadhi ya watu wanasema wachezaji wa zamani tulipata pesa na kuzitumia vibaya, sisi tunaamua tu kunyamaza lakini maisha ya wachezaji zamani yalikuwa ni magumu sana,” anasema.
Anasema kuna hatua ilifika klabu ya Simba iko mkoani na haina pesa, hawajui watasafiri vipi kufika eneo la tukio, watakula nini au watalala wapi.
“Hizi klabu zina wapenzi, hata Mo (Mohammed Dewji sasa ni mwekezaji wa Simba) kabla hajawa mfadhili amewahi kutusaidia mafuta.
“Nilimpigia simu nikiwa nahodha, timu iko Singida tunaelekea Mwanza, dereva akasema mafuta hayatufikishi Mwanza, alitusaidia mafuta, Abood ametusaidia sana mimi nikiwa nahodha pale Simba, kama nilivyosema ukiwa nahodha ni kiongozi.”
Anasema kuna muda timu iko mkoani hawana uhakika wa kula, wanalazimika kucheza mechi za ndondo, wanapewa laki tatu inagawanywa, maisha yanaendelea.
“Tumewahi kupiga ndondo Magu, Maswa, Kyela na maeneo mengi tu, ndiyo yalikuwa maisha yetu, tuliishi kwa ndondo, bonasi na wafadhili.”
Anasema waliwahi kukwama Mwanza timu ilikuwa haina pesa wakati huohuo wachezaji walikuwa wanapaswa kucheza mechi Zanzibar siku inayofuata kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati.
“Kocha wetu alikuwa James Siang’a sasa ni marehemu, viongozi wameshasema hawana pesa ya kutulipia ndege ili tuwahi kwenye mechi ile, tukapiga hesabu kwa timu zilizopo sisi uwezo wa kufika fainali tunao, hata tukiishia nusu bado tuna uhakika wa kupata pesa.
“Mimi, Hussein Marsha na Malota Soma akiwa nahodha-msaidizi tulimpigia mpenzi mmoja wa Simba anaitwa Bituro yuko Mwanza, tukamuomba aisaidie timu tiketi 12 tu za ndege, halafu tutamlipa.”
Anasema wachezaji ndiyo waliweka dhamana, yule jamaa akampigia meneja wa ATC usiku saa nne, wakafanikiwa kupata tiketi 12 za ndege kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam za siku iliyofuata saa 4 asubuhi, mechi inachezwa saa moja usiku Zanzibar siku hiyo hiyo.
“Kocha alipanga timu yake tukiwa Mwanza, tukaondoka wachezaji 11 na wa 12 ni kocha Siang’a kuja Dar ili tuwahi mechi Zanzibar usiku, wengine tukawaacha Mwanza wanasubiri ratiba ya treni ili kurudi.
“Sisi tulipofika Dar tukaunganisha bandarini tukachukua boti, siku hiyo bahari ilikuwa imechafuka, tulitapika sana, tumefika Zanzibar tuko hoi, hatuna sub, tukaunganisha uwanjani, tulicheza na timu moja dhaifu sana ya Somalia, tukatoka nayo sare, tulisemwa na kubezwa sana na mashabiki kwa matokeo yale, lakini hawakujua nyuma ya pazia kuna nini.”
Anasema mechi ya pili waliifunga Tusker hadi timu ikatinga fainali na wenzao waliowaacha Mwanza tayari walishaungana na timu Zanzibar baada ya kusafiri kwa treni kwa siku kadhaa na ile mechi Simba ilitwaa ubingwa na kupata pesa za kulipa deni la Bituro.
“Viongozi walikuja siku ya fainali kupokea pesa, maana yale mashi-ndano, chakula, usafiri wa ndani na malazi tulikuwa tunalipiwa na Cecafa, kuna changamoto nyingi sana wachezaji tumepitia zamani kwenye soka letu,” anasema.
MATOLA AOSHA
Mwameja anasema baada ya Malota Soma, Matola Suleiman ndiye alikuja kuwa nahodha msaidizi, sasa mwaka 1996 walitwaa ubingwa wa Cecafa na Matola ambaye sasa ni kocha msaidizi wa timu hiyo ndiyo alikuwa ameingia Simba.
“Mimi nilikuwa nahodha mkuu, lakini Matola akaniomba nimuachie akaoshe kwenye picha kwa kukabidhiwa kombe, nikamwambia sawa.
“Sasa meneja wetu Innocent Njovu baada ya kukabidhiwa bahasha ya pesa za washindi wa kwanza, akaichukua na kuipeleka kwa viongozi badala ya kuileta kwa wachezaji moja kwa moja kama ambavyo tulikubaliana,
“Hapo ndiyo mtafaruku ambao uliniondoa mimi Simba ulianzia, viongozi walisema kuna watu wametumika sana kwenye mechi na wengine hawatumiki sana, hivyo hawawezi kupata mgawo sawa wa pesa, tukasema hicho kitu hakipo, wale wasiotumika pia wana mchango wao na tumekubaliana tunapata mgao sawa sawa.
“Ikaonekana mimi nabishana na viongozi, sikutaka maneno ikabidi tu niondoke, huo ndiyo ukawa mwanzo wa mimi kustaafu, ila hawakujua sababu na sikucheza timu yoyote ile hadi leo.”
MIAKA 29 AKICHEZA SOKA
Safari ya Mwameja kwenye soka imedumu kwa miaka 29 hadi mwaka 2001 alipostaafu na kupishana na kipa Juma Kaseja, safari ambayo anasema ilikuwa ni safari nzuri na tamu kwake.
“Wenzangu nilioingia nao Simba walistaafu, wakaja wengine wakastaafu, wakaja wengine tena wakastaafu mimi nilikuwa bado nacheza, ingawa kipa ni mchezaji ambaye anaweza kudumu kwa muda mrefu uwanjani akiwa kwenye kiwango bora.
“Hata mimi nilistaafu nikiwa bado na kiwango changu tena kizuri tu, baada ya kuitumikia Simba kwa miaka 10, Coastal Union kwa miaka sita, Ndovu miaka minne, achilia mbali timu ya Bandari Tanga na timu ya kijijini nilikozaliwa ya Mwakidira Sports kwa miaka mingi, nimecheza soka kwa miaka 29,” anasema.
Anasema kila kitu katika safari yake hiyo kilibebwa na nidhamu na ukikipenda unachokitumikia na kufuata miiko, ukiongeza na kipaji unakifikia malengo,” anasema.
YANGA CHIMBUKO LA TANZANIA ONE
Katika safari hiyo ya soka, Mwameja alipachikwa jina la Tanzania One ambalo anasema alilisikia kwa mara ya kwanza akiitwa na wapenzi wa Yanga kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).
“Ilikuwa kwenye mechi ya Stars na Uganda, tunaingia Shamba la Bibi (Uhuru) nikasikia wananiambia wewe ndiyo Tanzania One, lakini kabla alikuwa akiitwa Ally Bushiri, baadaye Idi Pazi kidogo ndipo nikapewa mimi.”
Anasema tofauti za Simba na Yanga zipo lakini kuna baadhi ya wapenzi ukiachilia upenzi wao wanasema ukweli hasa kama mchezaji akiwa na kiwango na hayuko kwenye timu yake.
“Simba walikuwa wanasema Said Mwamba kizota yuko Yanga lakini ni bonge la mchezaji na Yanga wanasema Mwameja yuko Simba ila ndiyo kizingiti kwa timu yangu, Yanga ndiyo walianza kuniita Tanzania One, nakumbuka Simba waliwaambia kama mmemkubali nyinyi basi huyu ndiye Tanzania One halisi,” anasema.
MECHI NA TIMU YA GEORGE WEAH
Mwa-meja anasema Bushiri ndiye alikuwa mfano wake wa kuigwa, na ndiye alimhamasisha kupambana kwenye timu ya taifa baada ya kumueleza kwamba wao tayari umri umesogea hivyo akaze ili awe mbadala.