Sakho, Morrison waishika Morocco, Ibenge presha imepanda
SIMBA imetua nchini Morocco kisha kuanza safari ya kwenda Mji wa Berkane tayari kwa mchezo wao wa tatu wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini kuna mastaa wawili wa wekundu hao wameanza kuamsha vita upya kwenye kambi ya wapinzani wao.
Timu hizo zinakutana Jumapili ya Februari 27, mchezo wa tatu kwenye kundi lao D linaloongozwa na Simba wenye pointi nne wakati Berkane wakiwa na pointi tatu baada ya timu zote kucheza mechi mbili.
Mchezo wa kwanza Simba ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Asec Memosas kwenye Uwanja wa Mkapa, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini na USGN, nchini Niger.
Berkane watakaokuwa wenyeji wa Simba, mchezo wao wa kwanza waliifunga USGN mabao 5-3, kabla ya kupoteza kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Asec kwa mabao 3-1, hivyo mechi ya nyumbani itakuwa na vita kubwa ya kusaka pointi tatu.
Kocha wa Berkane, Mkongomani Florent Ibenge ameliambia Mwanaspoti kikosi chake kina mtihani mkubwa kuanza kutafuta dawa ya kuwatafutia tiba viungo washambuliaji wawili wa wekundu hao.
Alisema Pape Sakho na Bernard Morrison ndio mastaa wawili wanaotakiwa kutafutiwa tiba ya kuwatuliza wakati huu beki yao imekuwa na makosa makubwa.
“Simba ni timu kubwa, tunakabiliwa na mchezo mgumu dhidi yao, ukiangalia katika mechi zao mbili kuna watu ambao kama tunataka kushinda lazima tuwatafutie mbinu za kuwatuliza,” alisema Ibenge.
“Sakho (Pape) ni mchezaji mwepesi anayehitajika kuangaliwa sana kwa jinsi taarifa za mechi zao nilivyozipata lakini kuna yule Morrison (Bernard) ni mchezaji mzuri mwenye ubora akiwa uwanjani achilia mbali nidhamu yake, namjua vyema ni lazima tuwe na akili ya kuwazuia.
“Shida yetu ni makosa ambayo mabeki wangu wameyafanya kwenye mechi hizi mbili ni lazima tujue kucheza kwa utulivu kabla ya kukutana na Simba makosa haya ndio yametufikisha hapa kwa hizi mechi mbili,” alisema Ibenge.
Kocha huyo wa zamani wa AS Vita ya DR Congo, alisema hana wasiwasi na wachezaji wake wa eneo la ushambuliaji na kiungo juu ya ubora wao huku akicheka akihisi kiungo Clatous Chama anaweza kuwa na hatari katika kutoa siri za wachezaji wao na mbinu zao.
“Hapana Chama hawezi kutuathiri hata kama yuko Simba sasa, tunamkaribisha tu tena hapa Morocco tunatakiwa kucheza kwa ubora wetu na sio kuanza kumwangalia Chama ndio anajua hii timu kwa muda aliokaa hapa lakini hakuna tishio anaweza kuwa msaada mkubwa kwa wenzake wakati hatocheza.”
Hata hivyo, Chama hatocheza mechi hiyo na atakuwa jukwaani kutokana na kuzuiwa kikanuni. Nini maoni yako kuhusiana na kiwango cha Simba hii kimataifa,