Yanga inabeba hivi ubingwa.
IKIWA zimechezwa raundi 14 za Ligi Kuu Bara mambo yameanza kupamba moto, na hiki ndicho kipindi ambacho kila timu inakaa mguu sawa ili kumaliza vizuri msimu.
Vita kwenye ligi imeanza kugawanyika kwenye sura tatu ya kwanza ipo kwenye mbio za ubingwa ambazo zimeanza kupamba moto, vita nyingine ni ya timu ambazo zinalenga kumaliza kwenye nafasi za juu ikiwemo nne bora.
Vita ya mwisho ni kusalia Ligi Kuu na hii ni kati ya vita ngumu kwelikweli. Timu mbili ambazo zitamaliza msimu zikiwa mwishoni mwa msimamo zitashuka daraja moja kwa moja huku nyingine mbili zikikabiliwa na kibarua cha kucheza mechi za mchujo kusalia dhidi ya timu za Championship, ambapo shughuli huwa ni pevu.
Licha ya kuwa bado ni mapema, vipo viashiria ambavyo vinaibeba Yanga na kuiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa msimu huu. Hapa tunaigusa vita ya ubingwa ambayo imeanza kupamba moto. hata hivyo, hakuna mwenye uhakika wa kutwaa ubingwa hadi sasa licha ya uwepo wa viashiria hivi kutokana na idadi ya michezo iliyosalia.
UPANA WA KIKOSI
Licha ya kukosa huduma ya wachezaji kadhaa kwa vipindi tofauti, Yanga imeonekana kuwa na kundi kubwa la wale ambao wamekuwa wakibebeshwa majukumu ya kuziba pengo la wenzao. Mfano mzuri ni hivi karibuni Yanga iliondokewa na kipa namba moja, Djigui Diarra aliyeenda Cameroon na timu ya taifa ya Mali kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2021).
Hata hivyo, uwepo wa Aboutwaleeb Mshery uliifanya timu hiyo kutokuwa na pengo. Mshery alionyesha kiwango kizuri tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar wakati wa dirisha dogo la usajili na kipa huyo amekuwa mzuri kuanzisha mashambulizi kitu ambacho amekuwa akikifanya Diarra kiasi cha kutabiriwa mazuri.
Achana na eneo la golini safu ya ulinzi ya Yanga wakati huu ambao anakosekana Kibwana Shomary upande wa beki ya kushoto yupo Yassin Mustapha na David Bryson. Kukosekana kwa Feisal Salum kwenye michezo kadhaa iliyopita wameonekana wengine wakifanya vizuri akiwemo Saido Ntibazonkiza.
POINTI, REKODI
Japokuwa Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 36, tofauti ya pointi iliyopo baina yao na Simba ambao wapo nafasi ya pili ni tano huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa na pointi 31 kwenye michezo 15.
Ingawa ni pointi chache, lakini ni kati ya ishara ambazo zinaifanya Yanga kuonyesha kuwa imepania kubeba ndoo msimu huu, ikizingatiwa kwamba ni hivi karibuni kulikuwa na pengo la pointi 10 kati yao na watani wao hao, Simba.
Msimu uliopita kulikuwa na tofauti ya pointi nyingi baina ya timu hizo mbili, lakini kitendo cha Simba kuwa na idadi kubwa ya viporo kiliiangusha Yanga ambayo hata hivyo ilipoteza mwelekeo kwenye michezo dhidi ya Coastal Union ya Tanga ambao walipoteza kwa mabao 2-1 na dhidi ya Polisi Tanzania kwa satr ya 1-1.
Hii ni ishara tosha kuwa Yanga msimu huu inautaka zaidi ubingwa kuliko ilivyokuwa msimu uliopita ambapo walishuhudia Simba ikiutwaa kwa mara ya nne mfululizo.
Hadi raundi 14 ilizocheza Yanga imepoteza pointi sita tu kwenye michezo mitatu ambayo imetoka sare ambayo ni dhidi ya Namungo sare ya bao 1-1, Simba na Mbeya City zilizoisha kwa suluhu.
NGOME IMARA
Kati ya sifa za timu inayoweza kutwaa ubingwa ni pamoja na kuwa na safu imara ya ulinzi. Hii ina maana kuwa kama washambuliaji watashindwa kufunga, basi isiruhusu bao ili kuondoka uwanjani ikikusanya pointi hata kama ni moja. Ndani ya michezo 14 ambayo Yanga imecheza imeruhusu mabao machache zaidi - manne pungufu ya timu nyingine yoyote. Mabeki Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Shaaban Djuma, Yannick Bangala, Kibwana, Yassin na Bryason wamefanya kazi nzito na bado wanalo jukumu la kuhakikisha wanafikia lengo.
MABAO MENGI
Kasi ya ufungaji ya Fiston Mayele imestua tangu straika huyo alipotua Yanga ambapo amekuwa tishio akiifanya timu kuwa bora kwenye safu ya ushambuliaji tofauti na msimu uliopita. Yanga ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye ligi hadi sasa ikifunga 23, huku Mayele akitupia sita. Mbali na uwepo wa mshambuliaji huyo, kocha Nasreddine Nabi ana wigo mpana wa kufanya vizuri akiwa pia na mastaa wengine wanaombeba katika utupiaji kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ na hata Ntibazonkiza.